Polisi China kuendelea kushikilia machangudoa, wateja kwa miaka miwili

Sunday March 17 2019

 

Wakati wabunge wa China wakipendekeza kufutwa kwa vituo vya mafunzo ambako wanaouza miili na wateja wao wanaweza kuwekwa kwa hadi miaka miwili bila ya kufikishwa mahakamani, wanaharakati walitumaini kuwa siku za vituo hivyo zinahesabika.
Lakini sasa watalazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi.
Bunge la China (NPC) lilipitisha sheria moja wakati lilipomaliza mkutano wake wa mwaka Ijumaa iliyopita -- na sheria hiyo inahusu kufungua milango zaidi kwa wawekezaji wa kigeni.
Chini ya sheria hiyo ambayo imedumu kwa karibu miaka kumi, polisi wana mamlaka ya kukamata wanaofanya changudoa na wateja wao na kuwashikilia kwa kipindi cha hadi miaka miwili, wakiwa wamewaweka katika vituo vya "hifadhi na elimu".
Lakini wakosoaji wanasema hakuna suala la elimu katika vituo hivyo.
"Kunaweza kukawa na vikwazo ndani ya serikali dhidi ya kuondoa sheria hiyo, labda vikawekwa na polisi kwa kuwa kuvifuta kutaondoa mamlaka yao wa kushikilia watu bila ya kufikisha mahakamani," alisema Wang Yaqiu, mtafiti wa taasisi ya kushughulikia haki za binadamu ya Human Rights Watch.
Mwaka 2013, ushuhuda wa watu waliokuwa wanashikiliwa katika vituo hivyo uliokusanywa na taasisi ya Asia Catalyst, ambayo inatetea afya za makundi ya watu wachache -- ulibainisha hali mbaya ya maisha katika vituo hivyo.
Hiyo ni pamoja na kunyanyaswa, kufanyishwa kazi kinguvu, kulazimishwa kulipa fedha kwa ajili ya chakula na kulazimishwa kufanyiwa uchunguzi wa afya.
"Masuala yote haya ni kwa ajili ya fedha, mazungumzo ya mafunzo na elimu ni visingizio tu, ni njia ya kukusanya fedha kwa niaba ya serikali na polisi", mmoja wa wanawake hao aliiambia taasisi hiyo.
Shen Chunyao, mwenyekiti wa kamati ya sheria ya bunge la NPC, alisema mwezi Desemba kuwa "wakati umefika kwa vituo hivyo kufutwa".
"Katika miaka ya karibuni, matumizi ya mfumo wa kukamata watu na kuwashikilia kwa ajili ya mafunzo hayo yamepungua na vituo hivyo vimepigwa marufuku katika baadhi ya maeneo," alisema.
Mjadala kuhusu hali ya baadaye ya vituo hivyo uliibuka baada ya kamati hiyo ya sheria ya bunge kufuta mfumo wa "kuelimisha upya kwa kutumia kambi za kazi", unaojulikana kwa jina la "laojiao" mwaka 2013.
Kufunga kambi za kazi, zilizoanzishwa karibu miaka mia moja iliyopita kama njia ya haraka ya kushughulikia wavunjaji sheria wadogo, kulifunga pazia la picha mbaya na ya muda mrefu ambayo ilikuwa inakosolewa na makundi ya wapigania haki za binadamu na ambayo viongozi wa China walikiri kuwa hauna nafasi tena.
Lakini mamlaka ziliendeleza sheria ya kukamata changudoa na wateja wao na mwaka 2014 polisi ilkitangaza kuwa mcheza filamu maarufu, Huang Haibo angeshikiliwa kwa miezi sita baada ya kugundulika alimrubuni changudoa.
Suala hilo liliibua upinzani usio wa kawaida kutoka vyombo vya habari vya serikali vilivyohoji mfumo huo. AFP

Advertisement