Rafiki wa Boby Wine afariki baada ya kutekwa

Muktasari:

Msanii wa muziki nchini Uganda, Michael Kalinda maarufu Ziggy Wyne amefariki ikiwa ni siku moja tangu atekwe na kutelekezwa nje ya hospitali ya Mulago nchini humo.

Uganda. Msanii wa muziki nchini Uganda Michael Kalinda maarufu Ziggy Wyne amefariki dunia.

Ziggy Wyne ambaye ni rafiki wa karibu wa Mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulani   maarufu Boby Wine alifariki jana jioni Jumapili Agosti 4, 2019 katika hospitali ya Rufaa Mulago ambako ndiko alitelekezwa na watekaji waliomteka wiki moja iliyopita.

Katika tukio hilo la utekaji, msanii huyo alijeruhiwa kwa kutolewa jicho na kukatwa vidole ambapo baadaye watekaji waliamua kumtelekeza katika hospitali hiyo.

Hata hivyo, Bobi Wine alieleza siku ya Ijumaa hali ya msanii huyo ilionekana kuwa mbaya zaidi na ilipofika jana alifariki dunia.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, Fred Enanga amesema timu ya wachunguzi  kuhusu tukio hilo la kumteka Ziggy tayari imeshaanza kazi yake  ikiwemo kufika nyumbani kwa msanii huyo eneo la Gganda, Wilaya ya Wakiso.

 "Wachunguzi kutoka kituo cha Polisi Kawempe wameshaanza kazi yao ya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo la Ziggy Wyne, tunachokiomba ni ndugu kutoa ushirikiano pale watakapohitajika," alisema Enanga.