Rais Mnangagwa avijia juu vikosi vya usalama

Wednesday January 23 2019

 

Harare, Zimbabwe. Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema atavichunguza vikosi vya usalama baada ya kufanya vitendo vya ukandamizaji kwa waandamanaji wiki iliyopita.

Rais Mnangagwa aliandika katika ukurasa wa Twitter: "Vitendo vya vurugu na utovu wa nidhamu vilivyofanywa na vikosi vya usalama havikubaliki na vinaisaliti Zimbabwe mpya.”

Pia, alikosoa vikali maandamano yaliyogubikwa na fujo na uporaji, akieleza kwamba kila mmoja ana haki ya kuandamana, lakini maandamano hayo yalitawaliwa na vurugu.

Alisema waandamanaji walipora vituo vya polisi, wizi wa silaha na sare, uchochezi na vitisho vya vurugu, kwa mujibu wa Rais Mnangagwa. Ametoa wito wa kufanyika mjadala wa kitaifa miongoni mwa vyama vya kisiasa.

Watu 12 waliuawa na wengine 78 wanapatiwa matibabu kutokana na majereha ya risasi, kwa mujibu wa asasi ya haki za binadamu  iliorodhesha matukio zaidi ya 240 ya kushambuliwa na mateso.

Rais Mnangagwa alikiambia Kituo cha Taifa cha Utangazaji kuwa ziara yake nchini Urusi na Kazakhstan ilikuwa ya manufaa na itainufaisha Zimbabwe siku za usoni.

Polisi walimkamata katibu mkuu wa baraza la vyama vya wafanyakazi, Japhet Moyo na kumshtaki kwa kuratibu mgomo wa nchi nzima wa wiki iliyopita.

Pia, Serikali ilifunga huduma ya intaneti nchi nzima lakini mahakama ya juu iliamuru Serikali kurejesha huduma hiyo ikisema waziri wa ulinzi hakuwa na mamlaka ya kutoa amri hiyo bali ni rais pekee.

Advertisement