Rais Sri Lanka afananishwa na Hitler

Tuesday December 4 2018

Colombo, Sri Lanka. Waziri Mkuu wa Sri Lanka aliyeondolewa madarakani  amemfananisha Rais wa nchi hiyo na mtawala wa zamani wa Ujerumani dikteta Adolf Hitler huku akihaha kutaka arejeshwe kwenye nafasi yake, wiki sita tangu ulipoibuka mgogoro mkubwa wa kisiasa uliodhoofisha shughuli za Serikali.
Ranil Wickremesinghe alitoa maoni hayo leo ambayo ni makali kuwahi kutolewa yakimlenga mkuu wa nchi hiyo akiwa kwenye makazi ya waziri mkuu ambako amekataa kuondoka tangu alipofutwa kazi Oktoba.
"Rais anapaswa kuniteua mimi kuwa waziri mkuu kwa sababu nina idadi kubwa ya wabunge.”
"Namwambia wazi Rais asifanye mambo yake kama Hitler ambaye alikuwa anaipuuza Katiba. Hatuwezi kumruhusu kabisa afanye hivyo," alisema.
Rais Maithripala Sirisena alimfukuza kazi Wickremesinghe na akamteua Mahinda Rajapakse aliyewahi kuwa mkuu wa nchi hiyo aliyesifiwa kwa kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya majeshi ya Sri Lanka na kundi la Tamil Tigers waliotaka kujitenga mwaka 2009.
Hata hivyo, wakati Wickremesinghe akiwa na wafuasi wengi katika Bunge lililoshudia wabunge wakitwangana makonde wiki za hivi karibuni, mara mbili Rajapakse amepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.

Advertisement