Rais ajipanga kutangaza Serikali mpya Mali

Saturday April 20 2019

 

Bamako, Mali. Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, ameanza mazungumzo ya kuunda Serikali mpya baada ya Waziri Mkuu Soumeylou Boubeye Maiga na Serikali yake yote kujiuzulu  jana.

Taarifa kutoka ofisi ya rais inaeleza kwamba Rais Keita amepitisha kujiuzulu kwa waziri mkuu na mawaziri wake na kwamba atamtangaza waziri mkuu mpya pamoja na Serikali baada ya mashauriano na vyama vyote vya kisiasa nchini humo.

Inaaminika uamuzi huo unatokana na kuongezeka ghasia katika eneo la kati ya nchi hiyo, pamoja na mauaji ya halaiki mwezi uliopita wafugaji 160 wa kabila la Fulani walipouliwa na wanaodaiwa kuwa ni wawindaji wa kabila la Dogon.

Umoja wa mataifa(UN) unaripoti kwamba  mwaka mmoja uliopita mapigano kati ya wa-Fulani na wa-Dogon yamesababisha vifo watu 600.

Wiki mbili zilizopita kulikuwa na maandamano makubwa katika mji mkuu wa Bamako kulalamika dhidi ya serikali kushindwa kukomesha ghasia nchini humo.

 

Advertisement