Rais mteule Tshisekedi kuapishwa Alhamisi

Tuesday January 22 2019

 

Kinshasa,DRC. Maandalizi kwa ajili ya kuapishwa kwa rais mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  Felix Tshisekedi yanaendelea mjini Kinshasa .Sherehe hiyo iliotarajiwa kufanyika leo Jumanne imeahirishwa hadi Alhamisi.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Kinshasa  Msemaji wa Serikali inayoondoka madarakani Lambert Mende amesema kwamba uamuzi wa kusogeza mbele sherehe hizo ni kutokukamilika kwa maandalizi..

Hata hivyo alisema mahali  patakapofanyika sherehe hiyo bado hapajafahamika, lakini wafuasi wa chama cha UDPS cha Tshisekedi waliomba kiongozi wao aapishwe kwenye uwanja wa mpira  wa Kinshasa ili waweze kushiriki wengi.

Wakati huohuo,Polisi wamezuia wafuasi wa Martin Fayulu kukusanyika kwenye makao makuu ya chama chake alitakorajiwa kuwahutubia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la DW, Msemaji wa  Fayulu Eve Bazaiba amesema polisi walivamia mahali ambako Fayulu alitarajia  kuwahutubia wafuasi wake, na kulibeba jukwaa na vipaza sauti vilivyokuwa vimeandaliwa.

''Wamevikamata vyombo vyote na kuwakamata pia watu, na sijui wamewapeleka wapi.'' amelalamika Bazaiba na kuongeza, ''Nilipouliza kinachoendelea, nimeambiwa polisi wanacho kibali cha kuwazuia watu kuingia na kutoka.''

Advertisement

Licha ya kutawanywa na polisi baadhi ya wafuasi wa vuguvugu la upinzani la LAMUKA linalomuunga mkono Fayulu waliendelea kusubiri kuwasili kwa kiongozi wao kwenye makao makuu ya chama cha MLC.

Fayulu na wafuasi wake ambao wamepinga matokeo yaliotolewa na tume ya uchaguzi na kujitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo amesema kwamba ni lazima raia wa kongo wapewe haki zao.

''Tunachotaka ni kupata haki kulingana na matokeo ya uchaguzi, kwa sababu tuna uhakika kwamba tulishinda,'' amesema msemaji wa Fayulu Eve Bazaiba, na alipoulizwa watafanya nini kuhakikisha wanafanikiwa, amesema watazidi kukazana kwa sababu sheria iko upande wao.

Umoja wa Afrika (AU) umeahirisha ziara ya ujumbe wake iliyokua imepangwa kufanyika Jumatatu mjini Kinshasa, baada ya Mahakama ya Katiba kumtangaza Felix Tshisekedi kuwa rais wa DRC.

"Tume ya AU imepokea tangazo la Mahakama ya Katiba kuhusu matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais, uchaguzi wa Bunge na uchaguzi wa Magavana wa Desemba 30, 2018," Umoja wa Afrika umesema katika taarifa yake.

Mahakama ya Katiba ilidhibitisha  ushindi wa  Tshisekedi dhidi ya mgombea mwingine wa upinzani Fayulu, ambaye anapinga matokeo ya uchaguzi, na mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.

"Ikumbukwe kwamba ziara ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Au nchini DRC iliyokuwa imepangwa kufanyika  Januari 21 imeahirishwa," taarifa hiyo imeongeza.

Ujumbe huo ungeongozwa na rais wa sasa wa Umoja wa Afrika, Rais wa Rwanda Paul Kagame, na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat.

 

 

Advertisement