Rais wa Marekani ampigia simu mpinzani Libya

Saturday April 20 2019

 

Tripoli,Libya. Rais Donald Trump wa Marekani amezungumza kwa simu na kiongozi muasi, jenerali Khalifa Haftar.

Viongozi hao wawili wamezungumzia pia jinsi ya kubuni utawala wa mpito kuelekea mfumo wa kisiasa utakaodhamini utulivu na demokrasia.

 Vikosi vya Haftar vimeanzisha hujuma za kuuteka mji mkuu wa Libya Tripoli tangu mapema mwezi huu. Tripoli ndiyo makao makuu ya Serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Katika mazungumzo hayo ya jana, Trump na Haftar walijadiliana hatua za kupambana na ugaidi na haja ya kufikia amani na utangamano nchini Libya, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.

Taarifa ya Ikulu hiyo inasema kwamba Trump alilitambua jukumu muhimu la Jenerali Haftar katika kupambana na ugaidi na kulinda rasilimali ya mafuta ya Libya.

Marekani inaungana sasa na Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika kumuunga mkono Jenerali Haftar , ambaye mapambano yake ya kutwaa madaraka yanatishia kuirejesha tena Libya kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Advertisement

Ikulu ya Marekani haikusema kwa nini ilichelewa kutoa taarifa ya mazungumzo hayo ya simu kati ya Trump na Haftar, lakini wachunguzi wanasema uamuzi wa Trump kumsifia Haftar ni ushahidi wa kwa nini jenerali huyo muasi amekuwa na dhamira ya kuutwaa mji mkuu, Tripoli, unaodhibitiwa na Serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, anayetambuliwa na Umoja wa Mataifa.

 

Advertisement