Redio yazimiwa mitambo kwa kumhoji Besigye

Friday April 5 2019

 

Kampala, Uganda. Maofisa usalama nchini Uganda wanadaiwa kuzima matangazo ya radio Hope iliyopo katika Manispaa ya Kabale baada redio hiyo kuendesha mahojiano na kiongozi wa Chama cha Forum for Democratic Change, Dk Kiiza Besigye na viongozi wengine wa chama hicho.

Besigye na wenzake walikuwa wilayani humo katika kampeni ya kuimarisha uhai wa chama. Duru za habari zinasema mahojiano hayo yaliyotarajiwa kudumu kwa saa mbili lakini yalidumu kwa dakika 30 tu.

Mwendeshaji wa mahojiano hayo, Allan Twongyeirwe amesema leo Ijumaa Aprili 5, 2019 kuwa kabla ya kuanza mahojiano alipokea simu kutoka kwa Kamishna wa Wilaya ya Kabale, Darius Nandiinda akiamuru Besigye asihojiwe.

Alisema Nandiinda ameamuru askari wa Jeshi la Uganda (UPDF) kwenda katika milima ya Kihumuro Kabale, ambako ndiko ilipo mitambo ya kurushia matangazo na kuzima mitambo hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa FDC anayehusika na sera na utafiti, Dk Joseph Tindyebwa alisema redio hiyo ilizimwa wakati Besigye akielezea jinsi waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Hong Kong, Patrick Ho Chi-ping, alitolewa hivi karibuni hukumu ya miaka mitatu jela nchini Marekani baada ya kupatikana na hatia ya kutoa rushwa ya dola 500,000 kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Sam Kutesa na dola 2,000 kwa Rais wa Chad, Idriss Deby.

Besigye aliiambia Daily Monitor kuwa hata kabla ya mpango huo kuanza, aliambiwa na mwenyeji kwamba inaweza kuingiliwa.

Advertisement

 

 

Advertisement