Seneta ataka Jaji Mkuu wa Kenya anyimwe sakramenti

Nairobi. Seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata amesema ataliomba Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) limnyime sakramenti Jaji Mkuu David Maraga kutokana na matamshi yake mengi yanayokinzana na msimamo wa dini.

Jaji Maraga amependekeza umri wa mtu mzima uanzie miaka 16 badala ya miaka 18, kwa kuwa magereza nyingi zimejaa vijana wenye umri wa miaka 18 kwa makosa ya ngono.

“Maraga hafai kudai kuwa anatunga sheria, kazi ambayo inatekelezwa na wabunge ilhali yeye ni jaji. Nitatumia kila mbinu kuhakikisha anajiuzulu kwa sababu mapendekezo anayoyatoa kuhusu dhuluma za kimapenzi inazorotesha maadili katika familia. Inasikitisha anaunga mkono kupunguzwa kwa umri wa ngono ilhali inafaa kuongezwa hadi miaka 22,” akasema Kang’ata.

Seneta Kang’ata  alimkejeli Maraga kwamba hoja yake imelenga kutetea wazee wanaopenda kufanya ngono na watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka 18.

 “Kuna ukiukaji mkubwa wa haki kwa kujaza vijana magerezani kwa makosa ya kushiriki ngono na vijana wenzao kutokana na ashiki kubwa ya mahaba hasa wanapovunja ungo na kuingia utu uzima,” alisema Maraga wakati wa kuzindua warsha ya siku mbili kuhusu upatikanaji wa haki kwa wanaodhulumiwa kijinsia.

Lakini, Kang’ata alidai matamshi hayo ni njama ya kufanikisha mjadala wa kupunguzwa umri wa ujana kutoka miaka 18 hadi 16, hali ambayo itawapa wazee nafasi ya kuendeleza dhuluma dhidi ya watoto walio kati ya miaka 17 na 18.

Seneta huyo alisikitika kwamba matamshi ya Maraga kuhusu jinsi mswada wa kupunguza umri wa ujana ulivyokataliwa na Bunge ni kudhalilisha taasisi hiyo akisema kazi ya mahakama si kuunda sheria bali kuifafanua kortini.

Akizungumza na Taifa Leo, Kang’ata alisema matamshi ya Maraga yanaenda kinyume na dini ya Kikristo na anapanga kuwaongoza Wakristo na Waislamu kuandamana dhidi ya ofisi yake hadi ajiuzulu.