Serikali Mali yajiuzulu baada ya maandamano ya wiki mbili

Friday April 19 2019

 

By AFP

Waziri Mkuu wa Mali amejiuzulu pamoja na serikali yake baada ya kupingwa kutokasna na jinsi alivyoshughulikia vurugu zilizoibuka katikati ya nchi mwezi uliopita na kusababisha watu 160 kufariki dunia.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais Ibrahim Boubacar Keita inasema amekubali kujiuzulu kwa Soumeylou Boubeye Maiga na serikali yake, ikiwa ni wiki mbili baada ya wiki mbili za maandamano yaliyotokana na kuzuka kwa vurugu hizo.
Wabunge kutoka chama tawala na upinzani waliwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na serikali Jumatano, wakimlaumu Maiga na uongozi wake kwa kushindwa kutuliza vurugu.
"Waziri mkuu atatangazwa muda mfupi na serikali mpya itawekwa baada ya majadiliano na vyama vyote"; chama tawala na upinzani, taarifa hiyo ilisema.
Rais alisema Jumanne katika hotuba iliyorushwa na televisheni kuwa "alisikia hasira" za wananchi, bila ya kumtaja waziri mkuu.
Serikali ilijikuta katika shinikizo kubwa kutokana na jinsi ilivyoshindwa kudhibiti vurugu katika mkoa wa Mopti, na hasa mauaji ya watu 160 yaliyotokea Machi 23 wakati wakazi wa kijiji cha Ogossagou karibu na mpaka wa Burkina Faso waliposhambuliwa.
Watu wa ukoo wa Dogon -- ambao ni wawindaji na wakulima na ambao wana uhasama wa muda mrefu na kabila la Fulani ambao ni wafugaji kutokana na kugombea ardhi-- wanalaumiwa kwa kuhusika na mauaji hayo.
Wakati huo, mwandishi wa AFP alisema nyumba nyingi kijijini hapo zilichomwa moto na maeneo mengi yalijaa miili ya watu.
Wafulani pia wamekuwa wakituhumiwa kumuunga mkono Amadou Koufa ambaye anahubiri dini za mrengo wa kijihad.
Kundi linalojiita la kujilinda liliibuka katika jamii ya Dogon likitangaza kujipa jukumu la kulinda watu dhidi ya mashambulizi.
Lakini mgambo wanaoitwa Dan Nan Ambassagou, pia walitumia nguvu zao kuwashambulia Wafulani lakini jeshi hilo likavunjwa baada ya mauaji hayo ya watu wengi.
Maelfu ya watu waliandamana katika mitaa ya Bamako Aprili 5 kupinga mauaji hayo, wakiituhumu serikali kutochukua hatua zozote kuzuia.
Maandamano hayo yaliitishwa na viongozi wa Kiislamu, jumuiya inayowakilisha jamii ya Fulani, viongozi wa upinzani na taasisi za kiraia.
Mali imekuwa ikihaha kudhibiti vurugu tangu kundi la Waislamu wenye imani kali, linalohusishwa na kikundi cha Al-Qaeda kuteka eneo la kaskazini mwanzoni mwa Julai 2012.
Wakati wanamgambo hao wa kijihad waliondolewa wakati wa operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na Ufaransa kuanzia Januri 2013, maeneo mengi yamesalia bila ya utawala wa kisheria, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya amani mwaka 2015 ambayo yalilenga kuwaondoa kabisa wapiganaji wao wa Kiislamu.

Advertisement