Serikali ya Kenya yakataa kufuta tozo ya VAT katika mafuta

Wednesday September 12 2018

 

Nairobi, Kenya. Wizara ya Fedha imetetea uamuzi wake wa kutozuia utekelezaji wa tozo ya asilimia 16 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa ya mafuta.
Katibu mkuu wa wizara hiyo, Nelson Gaichuhie jana aliiambia Kamati ya Kudumu ya Seneti inayosimamia nishati kwamba hawajapokea barua yoyote kutoka mahakamani inayowamuru vinginevyo.
Gaichuhie aliiambia kamati hiyo kwamba hawajapuuza uamuzi wowote wa mahakama.
"Hatupuuzi wala kukataa kutii mahakama yoyote lakini ni hadi tutakapopewa barua, kwa sasa hatuwezi kufanya lolote,” alisema Gaichuhie.
Alisema kuahirisha utekelezaji wa sheria hiyo kwa miaka miwili zaidi hakutaweza kutatua tatizo lililopo.
"Labda tuifute kabisa kwa sababu kati ya sasa na mwaka 2020 hakuna kitakachobadilika," alisema na akaongeza kuwa Serikali iko hai na inasikiliza vilio vya umma na mashauriano mbalimbali yanaendelea.
"Kuna vikao baina ya Hazina na Bunge na tunatumaini kwamba ufumbuzi utapatikana,” alisema.
Lakini wakati Gaichuhie akisema hayo mbele ya kamati, Mahakama Kuu ilitoa amri mpya katika kesi ya kuidharau Mahakama inayomkabili bosi wake, Henry Rotich na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Robert Pavel Oimeke.
Katika uamuzi wake uliofikiwa kwenye Mahakama ya Kisumu, Jaji wa Mahakama Kuu, Fred Ochieng alipitisha uamuzi wa kukazia uamuzi wa muda wa kuzuia utekelezaji wa tozo mpya.
Mgogoro katika sekta ya mafuta unaendelea nchini Kenya tangu Septemba 1 serikali ilipoweka kodi ya asilimia 16 kwa mafuta na kusababisha hasira kubwa na upinzani kwa raia, huku bei za bidhaa mbalimbali zikipanda mara dufu.
Mahakama iliamuru taasisi husika kufuta kodi hiyo, lakini uamuzi huo umepuuzwa. Wapinzani wa kodi hiyo wanaendelea kuonyesha hasira zao.
Rais Uhuru Kenyatta anakabiliwa na upinzani mkubwa kufuatia hali hiyo. Kwa upande mmoja, anakabiliwa na shinikizo la kufuta kodi hiyo ambayo haiungwi mkono na wananchi wake. Kwa upande mwingine kuna hatari ya kutokea uhasama mkubwa kati ya Serikali yake na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambalo aliahidi kuweka kodi hiyo. IMF inaiomba Kenya kuongeza mapato yake ya kodi ili kulipa madeni.

Advertisement