Tajiri kuliko wote Algeria akamatwa kwa ufisadi

Muktasari:

  • Mualgeria ambaye ni tajiri kuliko wote nchini humo, Issad Rebrab amekamatwa siku chache baada ya Rais wa muda mrefu wa Algeria kutangaza kujiuzulu na mfanyabiashara huyo anatuhumiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu miamala ya fedha na ununuzi wa mitambo.

Mualgeria ambaye ni tajiri kuliko wote, Issad Rebrab amekamatwa na kuwekwa mahabusu kutokana na amri ya mwendesha mashtaka, vyombo vya habari vya Serikali vya nchi hiyo vimesema leo Jumanne, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa zinazomkabili.
Uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo umekuja baada ya kujiuzulu kwa Rais wa muda mrefu, Abdelaziz Bouteflika mapema mwezi huu baada ya wiki kadhaa za maandamano kupinga utawala wake uliodumu kwa miaka 20.
Rebrab, 74 ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa kampuni binafsi kubwa kuliko zote nchini Algeria inayojishughulisha na biashara tofauti ya Cevital, amelalala mahabusu kwa mujibu wa shirika la habari la APS.
Jarida la Forbes lilimuorodhesha Rebrab kama tajiri mkubwa kuliko wote Algeria na anayeshika nafasi ya tatu kwautajiri barani Afrika, akiwa na biashara zenye thamani ya dola 3.38 bilioni za Marekani mwaka huu.
Anatuhumiwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu uhamishaji fedha kwenda na kutoka nje.
Pia anatuhumiwa kuagiza kutoka nje mitambo ya mitumba licha ya kupewa msamaha wa kodi na ushuru kwa ahadi ya kununua mitambo mipya.
Mapema jana, Rebrab aliandika katika akaunti yake ya twitter kuwa alikwenda kwa hiyari yake kituo cha polisi kujadili kuhusu mitambo ambayo imekuwa ikishikiliwa kwenye bandari ya Algiers tangu Juni, mwaka jana.
Cevital, ambaye aliianzisha mwenyewe, imeajiri watu 12,000 na inajishughulisha na masuala ya elektroniki na chakula na katika miaka ya karibuni imenunua biashara nchini Ufaransa.
Kwa mujibu wa Forbes, Cevital pia ina miliki kiwanda kikubwa kuliko vyote duniani cha sukari ambacho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni mbili kwa mwaka. AFP