Trump atishia ‘kuiteketeza’ Iran

Muktasari:

Kauli ya Trump imekuja siku chache baada ya kusema kwamba hapendelei shinikizo la Marekani kwa Iran kugeuka vita huku Iran nayo ikipinga kuwapo kwa hali ya wasiwasi wa vita

NEW YORK, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump ameionya Iran kwamba itateketea iwapo vita vitazuka katika ya mataifa hayo mawili.

“Iwapo Iran inataka kupigana, huo ndio utakuwa mwisho rasmi wa taifa hilo,” alisema katika ujumbe wa Twitter jana Jumapili. “Msijaribu kuitisha Marekani tena.”

Marekani imepeleka meli zaidi za kivita na ndege katika eneo la Mashariki ya Kati katika siku za hivi karibuni.

Siku chache zilizopita, Rais huyo aliwaambia washauri wake kwamba hapendelei shinikizo la Marekani dhidi ya Iran kubadilika na kuwa vita.

Na alipoulizwa na waandishi wa habari Alhamisi iliyopita iwapo Marekani ilikuwa ikijiandaa kivita, Trump alijibu: Sidhani.

Iran pia imepinga madai ya kuwapo kwa hali ya wasiwasi. Siku ya Jumamosi waziri wa masuala ya kigeni wa taifa hilo, Javad Zarif alisema kuwa hakuna hamu ya vita.

“Hakutakuwa na vita kwa kuwa hatutaki vita na hakuna mtu ambaye anafikiria kuivamia Iran katika eneo hili,” Mohammed Javad Zarrif aliambia chombo cha habari cha Irna.

Hali hiyo inatokana na msuguano baada ya Iran kusitisha kwa muda makubaliano kuhusu mpango wa kinyuklia wa 2015, na kuonya kuendelea kuzalisha madini ya uranium ambayo hutumika kutengeza mafuta na silaha za kinyuklia.

Mpango huo ulilenga kusitisha vikwazo dhidi ya Iran ili isitishe mpango wake wa kinyuklia, lakini Marekani ilijiondoa katika makubaliano hayo mwaka uliopita.

Akiyataja makubaliano hayo kuwa mabaya, Trump baadaye aliiwekea tena vikwazo Iran.

Tehran imedaiwa kubeba silaha katika maboti katika eneo la Mashariki ya Kati, na wachunguzi wa Marekani wanaamini kwamba taifa hilo lilizishambulia meli nne za mafuta katika pwani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) madai ambayo Iran imeyakana.

Wakati hayo yakiendelea, Marekani imepeleka meli ya kivita inayobeba ndege kwa jina la USS Abraham Lincoln katika eneo hilo na imedaiwa kuwa kuna mpango wa kuwatuma wanajeshi 120,000 katika eneo hilo.

Wafanyakazi wa Kidiplomasia wametakiwa kuondoka nchini Iraq na Jeshi la Marekani limepandisha viwango vya hali ya tahadhari katika eneo hilo kutokana na ujasusi kuhusu vikosi vinavyoungwa mkono na Iran.

Wanajeshi wa Uholanzi na wale wa Ujerumani wanasema kuwa wamesitisha mazoezi yao ya kijeshi katika taifa hilo.

Kwa mujibu wa BBC, Jumapili Jeshi la Iraq lilisema kuwa roketi ilirushwa katika eneo salama linalolindwa sana katika mji wa Baghdad, ambalo linamiliki majumba ya Serikali na balozi za kigeni.

Inadaiwa kuwa roketi hilo lilipiga jumba moja lililoachwa karibu na ubalozi wa Marekani.

Hakuna majeraha yoyote yaliyoripotiwa na haijulikani ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

Kwengineko, Saudia imeishutumu Iran kwa kutekeleza shambulio la ndege isiyokuwa na rubani katika bomba moja la mafuta siku ya Ijumaa.

Inadaiwa kuwa waasi wa Houthi walitekeleza shambulio hilo kupitia maagizo ya Iran.