Tshisekedi adokezwa ufisadi kampuni ya madini

Muktasari:

  • Ni mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa DRC Rais Tshisekedi kusikiliza kero za wananchi

Kinshasa, DRC. Wafanyakazi wa kampuni ya Gecamines inayozalisha madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamemtaka Rais Felix Tshisekedi, kufanya ukaguzi kwani kuna ufisadi wa kutisha.

Wafanyakazi hao walilalamika mbele ya Rais Tshisekedi wakimtaka kufanya ukaguzi wa ndani wa kampuni hiyo na wamemtuhumu kiongozi wao kwa kuhusika na ufisadi na ubadhirifu wa mali za Serikali pamoja na kuchelewesha mishahara yao.

Katika taarifa yao walisema kampuni hiyo inaendeshwa kijanja tangu ikabidhiwe kwa mkuu wa shirikisho la wafanyabiashara katika jimbo la Katanga, Albert Yuma.

Wafanyakazi hao walisema kampuni hiyo kubwa ya madini tangu zamani imekuwa kitovu cha uchumi wa taifa hilo kubwa na tajiri Afrika lakini imeinufaisha kwa kiasi kikubwa familia ya rais mstaafu Joseph Kabila na Yuma ambaye ni mshirika wa karibu wa Kabila.

Kampuni hiyo inayozalisha madini ya cobalt, shaba na dhahabu kutoka Katanga Kusini-Mashariki mwa DRC imekuwa chini ya usimamizi wa Yuma, tangu mwaka 2010.

Hata hivyo hakuna tamko lolote kutoka kwa uongozi wa kampuni hiyo kuhusu tuhuma hizo wakati wafanyakazi hao wakisubiri uamuzi wa Rais Tshisekedi.