Tume yadai wananchi wamekubali el-Sisi atawale mpaka 2030

Muktasari:

  • Tume ya Uchaguzi Misri imesema kwamba wapiga kura asilimia 90 wamekubali Rais atawale mpaka 2030

Cairo,Misri. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema wapiga kura asilimia 90 wamekubali kumuongezea muda wa utawala Rais  wa nchi hiyo, Abdel Fattah el-Sisi  ambaye atatawala mpaka 2030.

"Haya mabadiliko yanafanyika haraka iwezekanavyo kwenye katiba yetu, kama wananchi walivyotaka hatuwezi kuwaangusha,’’amesema mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo, Lasheen Ibrahim akihutubia moja kwa moja kupitia luninga ya taifa.

Alisema zaidi ya wapiga kura ya maoni  23.4 milioni walipigia kura mabadiliko ya katiba hiyo kumruhusu kiongozi huyo kutawala mpaka 2030.

Watu wengi walionekana kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kupiga kura ambapo mamia ya wazee kwa vijana walijumuika pamoja.

Mmoja wa wananchi hao, Haja Khadija (63) amesema amepiga kura kwasababu ya usalama na utulivu wa nchi. "Tunampenda el-Sissi. Amefanya mengi. Ametuongezea malipo ya uzeeni."

Kituo cha televisheni ya taifa kinasema Rais  el-Sissi alipiga  kura katika mkoa wa Heliopolis karibu na kasri la Rais mjini Cairo.

Vyombo vya habari vinavyoelemea upande wa Serikali vimekuwa vikifanya kampeni zao tangu wiki kadhaa na kuitaja kura hiyo ya ndio wajibu mkuu wa kitaifa.

Kuanzia mapema  Aprili  mji mkuu wa Misri ulijaa mabango na maandishi yanayowahimiza wapiga kura waunge mkono mageuzi.

Bunge linalodhibitiwa na wafuasi wa el-Sissi limeunga mkono kwa wingi mageuzi. Sauti 22 tu ndizo zilizopinga na moja kutoelemea upande wowote kutoka jumla ya wabunge 554 waliohudhuria kikao hicho. Siku ya pili yake tume ya uchaguzi ikatangaza upigaji kura.

Kura ya maoni inafanyika miaka minane baada ya vuguvugu la kudai demokrasia kumaliza utawala wa miongo mitatu wa Hosni Mubarak na miaka karibu sita baada ya el-Sissi kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'oa madarakani Rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia huru, Mohammed Morsi.

Makundi mawili ya kimataifa, Human Rights Watch na halmashauri ya kimataifa ya wanasheria yameihimiza Serikali ya Misri ibatilishe mageuzi hayo.