UN: Vurugu zinaweza kuibuka tena DRC

Muktasari:

  • Wachunguzi wa UN wamesema kuwa ghasia zilizotokea kati ya Desemba 16 na 18 zilikuwa zimepangwa

Kinshasa, DRC. Ripoti ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa (UN) imesema ghasia zilizotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika kipindi cha mwaka uliopita ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Ripoti hiyo imesema takriban watu 500 waliuawa ikiwemo familia kuchomwa moto ndani ya nyumba zao na mtoto wa miaka miwili kutupwa ndani ya tanki la maji machafu.

Ghasia za kikabila zilitokea pia wakati jamii moja ilipotaka kuzika mmoja wa viongozi wao wa kitamaduni katika ardhi ya jamii nyingine.

Pia kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na UN imeonyesha kuwa vurugu zinaweza kuibuka tena wakati wowote.

Jamii ya kabila la Batende walivamia na kushambulia vijiji vya wa Banunu, na watu wachache tu ndio waliofanikiwa kutoroka.

Taarifa hiyo, imeongeza pia mamlaka katika eneo la Yumbi, jimbo la Mai-Ndombe, Magharibi mwa DRC, zilishindwa kuwajibika kwa kuwalinda raia.

Idadi ya watu waliokufa inaweza kuwa zaidi ya 535, iliyowekwa katika ripoti hiyo ya uchunguzi. Timu hiyo ya uchunguzi ya UN iliweza kuvifikia vijiji vitatu kati ya vinne, wakati mashambulizi yalipopamba moto.

Hata hivyo tayari aliyekuwa kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi ametangazwa kuwa mshindi na sasa ndio Rais wa nchi hiyo.