UN yapoteza wafanyakazi 22 ajali ya ndege Ethiopia

Monday March 11 2019

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Nairobi, Kenya. Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) limetoa pole kwa nchi, familia na ndugu waliopoteza jamaa zao 157 kwenye ajali ya ndege ya Shirika la Ethiopia iliyotokea jana Jumapili na kubainisha kuwa walikuwamo wafanyakazi wake 22.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo Jumatatu, Machi 11,2019 imeeleza wafanyakazi hao kutoka maeneo tofauti duniani walikuwa wanakuja Nairobi kuhudhuria mkutano wa Shirika la Mazingira (UNEA).

Akisoma taarifa hiyo katika kikao cha dharura cha zaidi ya wajumbe 4,700 wanaohudhuria mkutano huo, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UN Habitat), Maimunah Sharif amesema UN inaungana na familia pamoja na nchi zilizopoteza jamaa zao kuomboleza vifo hivyo.

"Tumepoteza wafanyakazi 22. Ni pigo kubwa kwetu. Walikuwa wanakuja kuungana nasi hapa. Umoja wa Mataifa unatoa pole kwa familia na ndugu waliopoteza wapendwa wao," amesema Maimunah.

Waalikwa wanaohudhuria mkutano huo walisimama kwa dakika moja kutoa heshima kwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Tangu asubuhi leo, baada ya kuthibitika kwa vifo hivyo, bendera ya Umoja wa Mataifa inapepea nusu mlingoti.

Advertisement

Kuanguka kwa Boing 737-800 mali ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kusababisha vifo vya abiria na wafanyakazi wote waliokuwamo kumezua simanzi duniani.

Advertisement