Uingereza yaweza kusitisha Brexit

Tuesday December 4 2018

London, Uingereza. Serikali ya Uingereza ina uwezo kwa kauli ya pamoja kusitisha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) maarufu kama Brexit, wamesema washauri waandamizi wa kisheria wa EU.
Katika ripoti iliyoandaliwa kwa ajili ya Mahakama ya Ulaya yenye makao yake Strasbourg, mkuu wa mawakili alisema Uingereza inaweza kuachana na mchakato huo uliochukua miaka miwili chini ya Ibara ya 50.
Uingereza ilidai kwamba Ibara ya 50 inaweza tu kukamilika kwa makubaliano ya nchi 27 zilizobaki wanachama wa EU.
Akitangaza uamuzi huo Jumatatu, mkuu wa mawakili Campos Sanchez-Bordona alisema kwamba Ibara ya 50 inaruhusu uondoaji wa moja kwa moja wa taarifa ya kusudio la kujiondoa EU.
Majaji sasa watapaswa kuamua ikiwa wakubaliane na ushauri wa wakili mkuu kama wanavyofanya katika mashauri mengi.
Ikiwa watafanya hivyo, italipatia Bunge la Uingereza nafasi nyingine ambayo ni kuilazimisha Serikali iweke mkono. Zikiwa zimesalia wiki 16 tu kabla ya tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa Ibara ya 50 Machi 29, fursa za chaguo zinazidi kwisha ikiwa Bunge litakataa mpango wa Brexit uliowasilishwa na Waziri Mkuu Theresa May.
Jo Maugham, mmoja wa walalamikaji katika kesi hiyo alikubaliana na maoni ya wakili mkuu akiwahimiza wabunge wa Uingereza kuonyesha dhamiri zao na kutekeleza wajibu kwa manufaa ya nchi.
"Hayo ni kati ya maamuzi ambayo Uingereza inaweza kufanya kwa kauli moja bila ya kuwapo haja ya kusubiri idhini kutoka wanachama wengine wa EU. Uamuzi huo utaweka mustakabali wetu kuwa katika mikono ya wawakilishi wetu waliochaguliwa," alisema.

Advertisement