Upinzani wapaza sauti uchaguzi Afrika Kusini

Muktasari:

  • Wakati wananchi wa Afrika Kusini wanajiandaa kumchagua Rais wao mpya ndani ya wiki moja, chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kinasema iwapo kitashinda kitatekeleza maoni ya Rais wa kwanza mweusi Nelson Mandela aliyetaka nchi hiyo kumjumuisha kila mmoja.

Pretoria. Afrika Kusini. Uchaguzi wa Afrika Kusini utafanyika Jumatano wiki ijayo na Rais anayemaliza muda wake, Cyril Ramaphosa anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.

Kulingana na uchunguzi wa awali, chama tawala cha ANC kinaongoza kwa asilimia 50 ya kura.

Uongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance umesema sera zake zinaangazia yale aliyoyaamini Rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo, Nelson Mandela na unashutumu chama tawala cha ANC kinachopewa nafasi kubwa kwenye uchaguzi kuwa kimeshindwa kusimamia maoni ya kiongozi huyo wa zamani.

Kwa upande wake, Julius Malema kiongozi wa chama cha upinzani cha EFF, ameishutumu ANC kwa kuwatelekeza wakazi wa vijijini.

Akihutubia mkutano wa kampeni Jumatano katika uwanja wa Alexandra, Malema alisema: "ANC ilifanya nini? Hakuna! Walijihusisha tu na kuiba fedha. Hii ndiyo sababu chama cha EFF kinasema ni lazima tuwanyang'anye mashamba wakulima bila fidia na kuwapa wenyeji wa Alexandra ili waweze kujenga nyumba zao."

Uchaguzi huu unaonekana kuwa na ushindani, lakini Rais Ramaphosa bado anapewa nafasi kubwa ya kushinda.