Urusi iko tayari kuboresha uhusiano na Marekani

Monday March 25 2019

Urusi. Serikali ya Urusi imesema iko tayari kuboresha uhusiano wake na Marekani lakini ni jukumu la nchi hiyo kuanza kulifanyia kazi jambo hilo.

Kauli ya Urusi inakuja ikiwa ni muda mfupi tangu uchunguzi uliokuwa na nia ya kubaini iwapo Rais Donald Trump na wasaidizi wake wa uchaguzi kwa kushirikiana na Urusi walihusika kuvuruga uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka 2016 uliomuweka madarakani Trump.

Urusi imezungumzia uchunguzi wa mwendesha mashitaka maalumu Robert Mueller baada ya ripoti yake fupi iliyotolewa Jumapili ambapo Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr amesema, hakuna ushahidi wa kiuchunguzi unaoonyesha kuwa Rais Trump kwa namna yoyote alizuia haki isitendeke na kumfanya ashinde urais wa mwaka 2016.

Muda mfupi kabla ya Rais Trump kuingia madarakani, mashirika ya kiintelijensia ya Marekani yaliwahi kuripoti kwamba, Urusi iliingilia matokeo ya Urais ya nchi hiyo, kwa njia ya kampeni ya kudukua barua pepe na propaganda za mtandaoni lengo likiwa ni kutengeneza chuki ndani ya Marekani.

Akizungumzia juu ya kuimarika kwa uhusiano wa Urusi na Marekani baada ya ripoti ya Mueller, Peskov amesema Rais Vladmir Putin alikwishaweka wazi nia yake ya kuboresha uhusiano na nchi hiyo akikumbushia mkutano kati ya marais hao uliofanyika nchini Finland  Julai mwaka uliopita.

Advertisement