VIDEO: Wanajeshi Gabon wafanya jaribio la kumpindua Rais Bongo

Monday January 7 2019

Gabon. Kundi la wanajeshi wa Gabon wametangaza kuipindua Serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Ali Bongo.

Kwa mujibu wa ripoti ya BBC leo Jumatatu Januari 7, 2019 wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita wanashika doria kwenye barabara za mji mkuu wa Libreville.

Amri ya kutotoka nje imetangazwa kupitia kituo cha redio ya Taifa ambacho kimedhibitiwa na wanajeshi hao kuanzia saa 11 alfajiri.

Katika matangazo yao redioni, wanasema kumekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wa Rais Bongo kuongoza Taifa hilo kwa madai kwamba afya yake si nzuri.

Wanajeshi hao wamesema wamechukua hatua hiyo kurejesha demokrasia. Wametangaza kwamba wataunda Baraza la Ukombozi ambalo ndilo litakaloongoza Serikali.

Wamekosoa hotuba iliyotolewa na Rais Bongo Desemba 31, wakisema mawazo yake hayakuwa kwenye mtiririko mzuri na sauti yake ilikuwa dhaifu, jambo ambalo linaonyesha kwamba afya yake si nzuri.

Rais Bongo amekuwa nje ya nchi akipata matibabu nchini Morocco kwa miezi miwili sasa kutokana na maradhi ambayo hayajabainishwa wazi.

Familia ya Bongo imetawala Taifa hilo kwa miaka 51 iliyopita huku ikituhumiwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa kutokana na rasilimali za Taifa hilo.

Rais Bongo alichukua madaraka mwaka 2009 kutoka kwa baba yake, Omar Bongo ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 40. Alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2016, uchaguzi huo uligubikwa na ghasia na udanganyifu.

Advertisement