Bendera zazua taharuki Ethiopia, Waziri mkuu aonya

Muktasari:

  • Vurumai ilihusu suala la kupandisha bendera zinazoashiria makundi ya harakati za upinzani ya Oromo

Addis Ababa, Ethiopia. Mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, uko katika hali ya taharuki baada ya kutokubaliana kuhusu matumizi na mahali pa kuweka bendera maalumu katika maeneo mbalimbali, vyombo vya habari vya serikali na binafsi vimeripoti.
Gazeti la Addis Standard limesema taharuki hiyo ambayo imezua ugomvi na makabiliano katikati ya jiji ulihusisha makundi ya vijana kutoka mkoa wa Oromia na wakazi wa jiji.
“Vurumai ilihusu suala la kupandisha bendera zinazoashiria makundi ya harakati za upinzani ya Oromo yaliyotaka kupaka rangi vibaraza, barabara, nyumba na maeneo mengine yenye rangi kama hizo nyekundu na kijana huku manjano ikiwa katikati kazi iliyofanywa na vijana kutoka Oromia huku wakazi wa jiji walikuwa wanataka kuwazuia.
“Mchakato kama huo mara ya kwanza ulifanywa na wakazi wa Addis Ababa waliopaka rangi zilizokolea za kijani, manjano na nyekundu, kwenye bendera nyingine isiyo rasmi wakati wa shamrashamra za kuupokea uongozi wa kundi la Patriotic Ginbot 7 mwishoni mwa wiki iliyopita,” gazeti la Addis Standard lilieleza.
Akizungumzia matukio hayo, Waziri Mkuu Abiy Ahmed alinukuliwa na shirika la utangazaji la serikali la Fana akitoa onyo dhidi ya matumizi ya ghasia wakati mjadala ndio unapaswa kutumika kupata ufumbuzi.
Shirika la Fana liliongeza kwamba Abiy alilaani kile alichosema ni jaribio la kuchochea ghasia kwa kisingizio cha bendera.
“Haki ya uhuru wa kujieleza inahusisha pia bendera,” alinukuliwa akisema na akaongeza: "Hatupaswi kuvitenga vyama vya kisiasa vilivyorudi vikitokea nje ya nchi."
“Kwa kuwa hataweza kupatikana mshindi, lazima tushirikiane kwa kutatua tofauti baina yetu kwa majadiliano,” alisisitiza Abiy.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi la Shirikisho Jamal Zeinu imeripotiwa ametoa wito wa kuwepo utulivu na akasisitiza kwamba jeshi hilo litafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anaimarisha amani na utulivu.