Waandamana wakitaka kuharakishwa mabadiliko Algeria

Muktasari:

  • Rais Bouteflika aliahirisha uchaguzi uliokuwa ufanyike Aprili 18 mwaka huu

Algers, Algeria. Mamia ya wananchi Algeria wameandamana nchi nzima kutaka mabadiliko ya kisiasa ya haraka, baada ya rais wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika kutangaza kwamba hatogombea tena urais muhula wa tano.

Licha ya kutangaza kuachana na kuwania urais huo, Rais Bouteflika hakutangaza kujiuzulu.

Makundi ya watu yalijikusanya kwenye miji kadhaa na televisheni ya Ennahar iliripoti kwamba wafanyakazi walianza mgomo uliosimamisha  shughuli za kazi katika Bandari ya Bajaia kwenye Bahari ya Mediterania.

Bouteflika (82) alitangaza uamuzi wake wa kutokugombea tena baada ya shinikizo la maandamano nchini mwake kutaka aachie madaraka.

Habari za ndani zimearifu kuwa mwanadiplomasia mahiri wa Algeria, Lakhdar Brahimi, aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Algeria, ataongoza baraza litakalosimamia kipindi cha mpito na ambalo pia litatayarisha Katiba mpya na kupanga tarehe ya uchaguzi.