Wabunge wadhamiria kumng’oa Ruto

Tuesday March 26 2019Naibu Rais nchini Kenya, William Ruto

Naibu Rais nchini Kenya, William Ruto 

Nairobi,Kenya. Huku mjadala kuhusu vita dhidi ya ufisadi ukizidi kupamba moto, kambi tofauti za kisiasa zinazidi kushambuliana kuhusu jinsi vita hivyo vinavyoendeshwa.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wabunge tayari wanawazia kumng’oa Naibu Rais, William Ruto huku Seneta wa Siaya, James Orengo akitaka kiongozi huyo aondoke kwa kutofautiana na Rais.

Wabunge kutoka maeneo ya Mlima Kenya na Ukambani wameeleza kughadhabishwa kwao na Ruto, wakionyesha dalili za kuwasilisha muswada wa kutokuwa na imani naye.

Wakiwa katika eneo la Bunge la Kathiani Jumamosi, zaidi ya viongozi 10 walimvamia Naibu Rais kuhusiana na jinsi ambavyo amekuwa akikosoa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusu jinsi inavyoendesha vita dhidi ya ufisadi, baadhi yao wakipendekeza kuwa itakuwa afadhali kumng’oa madarakani.

 “Serikali ni ya Uhuru, si ya Uhuru na mtu mwingine, Urais haugawanywi, sisi hatuna Rais wawili. Wakati huu Rais  si mwizi, mwizi yuko kitandani karibu naye,” alisema mbunge wa Kangema, Muturi Kigano.

Mbunge mwenzake wa Kathiani, Robert Mbui naye alimtaka Rais Kenyatta kumfuta kazi Ruto.

 “Ninataka kuuliza Rais, si unajua yule ‘mshirika wa kisiasa wa karibu zaidi’ wako ni nani? Rudisha huyu mtu nyumbani ama utuambie tumng’oe mapema ili ufanye kazi,” alisema Mbui.

Wabunge hao walikuwa wakizungumza katika hafla iliyohudhuriwa na wabunge kadhaa wakiwamo Maina Kamanda (Starehe), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Paul Koinange (Kiambaa), Dan Mwachako (Wundayi) na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Dennis Waweru.

Viongozi hao walimshutumu  Ruto kuhusu sakata la pesa zinazodaiwa kuporwa kwenye miradi ya mabwawa ya Kimwarer na Arror, kufuatia matamshi yake kuwa si Sh21 bilioni zinazokosekana ila ni Sh7 bilioni zinazotiliwa shaka.

Matamshi ya mbunge huyo yaliungwa mkono na Mwachako ambaye alisema “Yule atakayetajwa kuwa amekula pesa za mwananchi, mwacheni akae pembeni uchunguzi ufanyike.”

Koinange, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu usalama naye alisema pesa zote za umma ambazo zimeporwa zitarejeshwa.

“Kama Ruto anamtambua Uhuru Kenyatta kuwa Rais wa Kenya kwa kweli lazima pia ajitokeze kusema kuna wizi. Lakini kama Uhuru anasema hivi na yeye anasema vingine, wanafanya kazi pamoja kweli? Tunataka Uhuru asiogope. Ukiwa na number two lazima ufanye ile kazi unayotaka naye awafanyie wananchi, ukiacha hivyo unakuwa msaliti.”

 

 

Advertisement