Wakenya wanamtafuta Rais Kenyatta mitandaoni

Muktasari:

  • Wadai Rais huyo ametoweka tangu aliporejea kutoka ziarani nchini China

NAIROBI. Wakenya wamekuwa wakitumia mtandao wa kijamii wa Twitter kuuliza maswali kuhusu mahali aliko Rais Uhuru Kenyatta.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard, Kenyatta aliondoka nchi humo Aprili 23, kukutana na Rais wa China, Jinping na inasadikiwa kuwa alirejea nyumbani kimya kimya siku ya Ijumaa Mei 3.

Hata hivyo, taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo Jumatatu Mei 13, kupitia mtandao wa Twitter ilisema Rais Kenyatta yupo nchini na kwamba kutoonekana hadharani hakumaanishi kwamba hayupo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Rais Kenyatta yupo ofisini na kwamba anaendelea na kazi zake kama kawaida.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa Rais Kenyatta hajaonekana hadharani kitendo kilichozua gumzo katika mtandao wa Twitter ambako walitumia hashtag ya #FindPresidentUhuru.

Katika mtandao huo, baadhi yao walijaribu kuelezea kwa nini rais hajaonekana hadharani kwa majuma mawili huku wengine wakidai kuwa alifuta akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii na kisha akaelekea ziara ya China kutafuta mkopo ambao hata hivyo hakuupata.

Awali Gavana wa Jimbo la Machakos lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Nairobi, Dk Alfred Mutua alinukuliwa na vyombo vya habari akimtetea Rais Kenyatta kwa kutoonekana hadharani kwa muda.

''Rais ni meneja mwenye shughuli nyingi kwa hiyo anahitaji muda wa kufanya mikutano, kupokea taarifa muhimu za Serikali na kushughulikia masuala ya uchumi wa nchi,'' alisema Mutua.

Aliongeza kuwa anashangaa kusikia watu wakiulizia kwa nini Rais hajaonekana hadharani tangu arejee kutoka ziara ya China.