Wakenya watajwa kuhusika na ugaidi

Saturday January 19 2019

 

Nairobi.Kenya. Wachunguzi nchini Kenya wanasema kuna uwezekano baadhi ya washambuliaji wa hoteli ya DusitD2 nchini humo walikuwa raia wa Kenya.

Kijana wa miaka 26 Ali Salim Gichunge ametajwa  kuwa miongoni mwa watuhumiwa waliohusika na shambulio hilo.

Maofisa wa usalama wametoa  taarifa chache juu ya timu ya wanamgambo watano waliofanya shambulio hilo na kusababisha vifo vya watu 21.

 Al-shabab walidai kuhusika na shambulio hilo. Kundi la Al shabaab  lina mfungamano na kundi la al-Qaeda.

Washambuliaji wote sita waliuliwa  wakati wa shambulio hilo kama alivyosema Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika hotuba yake siku ya pili baada ya tukio hilo.

 Wakati huo huo, polisi wamesema  wamewakamata baadhi ya wahusika wanaodaiwa kushirikiana na waliofanya shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa polisi mmoja wa watuhumiwa alikamatwa Ruaka, Kaskazini mwa Nairobi ambako mmoja wa magaidi anadaiwa kuwa aliishi kabla ya shambulio hilo.

Mwingine alikamatwa  Eastleigh, eneo la mji mkuu Nairobi wanakoishi raia wenye asili ya Somalia. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Right Watch pia limeshauri Serikali kuepuka matumizi yoyote mabaya wakati wa uchunguzi.

Shirika hilo lisilo la kiserikali limekumbusha kuwa katika siku za nyuma jitihada za Kenya za kukabiliana na kudorora kwa usalama ziligubikwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hasa dhidi ya jamii ya raia kutoka Somalia .

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba washambuliaji hao wameangamizwa na kwamba operesheni ya uokoaji imekamilika.

Kenya imekuwa ikilengwa na kundi la al Shabab tangu Oktoba 2011, wakati taifa hilo lilipotuma vikosi vyake nchini Somalia kupambana na kundi hilo.

Watu 28 waliojeruhiwa walilazwa katika hospitali mbalimbali huku wengine 19 wakiwa hawajulikani waliko, Shirika la Msalaba mwekundu limesema.

Idadi ya watu waliofariki katika shambulio hilo  imeongezeka hadi kufikia  21 kwa mujibu wa Serikali.

Advertisement