Wanafunzi vyuo vikuu Algeria wapewa likizo ya mapema

Muktasari:

  • Likizo hiyo imetolewa wakati vuguvugu la maandamano ya kumpinga Rais Bouteflika likiwa limepamba moto baada ya wananchi kuonekana kumchoka Rais huyo mwenye umri wa miaka 82 ambaye anaugua kiharusi

Algiers, Algeria. Wizara ya elimu ya juu nchini Algeria imewapa  likizo ya lazima wanafunzi wa vyuo vikuu katika hatua ya kujaribu kuyadhoofisha maandamano ya kumpinga Rais Abdelaziz Bouteflika (82) kugombea muhula wa tano.

Wizara ya elimu ya juu imetangaza kwamba likizo hiyo itaanza leo Jumapili na kuendelea hadi Aprili 4.

Kwa kawaida likizo hiyo huwa ya wiki mbili na huanza Machi  21 hadi Aprili 5 kila mwaka. Walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu kadhaa wameanza mgomo, huku wengine wakiahidi kuanza mgomo leo hii Jumapili.

Rais Bouteflika ambaye ni nadra kuonekana hadharani tangu augue kiharusi mwaka 2013 ameahidi kutokamilisha muhula wake iwapo atachaguliwa tena katika uchaguzi wa Aprili 18, lakini wanafunzi wa vyuo vikuu wanaipinga hatua hiyo.

Uamuzi huo wa Wizara ya Elimu ya Juu umefikiwa baada ya maelfu ya watu kuandamana katikati ya mji mkuu Algiers kwenye maandamano makubwa yaliyowahi kutokea kwenye mji huo mkuu katika kipindi cha miaka 28 kupinga utawala wa miaka 20 wa kiongozi huyo wa zamani.

Maelfu ya wanafunzi wameshiriki kwenye maandamano ya kumpinga Bouteflika tangu kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alipotangaza nia yake ya kugombea muhula wa tano katika uchaguzi wa Urais unaotarajiwa kufanyika April 18.

Katibu Mkuu wa wizara ya elimu ya juu nchini Algeria, Abdelhafid Milat, ameukosoa uamuzi wa kutangaza mapema likizo hiyo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kabla ya wakati wake.

Ameliambia shirika la habari la Ujerumani kwamba ni jambo la kushangaza katika historia ya elimu ya juu nchini Algeria. Milat amesema jumuiya ya elimu ya juu itakutana na kuamua juu ya majibu kufuatia hatua hiyo ya wizara ya elimu ya juu.

Maandamano hayo yamekuwa ya amani tangu yalipoanza zaidi ya wiki mbili zilizopita katika nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini.

Hata hivyo inadaiwa raia zaidi ya 100 walijeruhiwa wakati walipopambana na maofisa usalama katika mji mkuu wa Algeria, Algiers kwenye maandamano ya siku ya Ijumaa.

Baadhi ya waandamanji walijeruhiwa kwa kupigwa mawe na risasi za mpira wakati wengine walipata majeraha kutokana na kupuliziwa gesi ya kutoa machozi na vikosi vya usalama.

Taarifa zaidi zinaarifu kuwa waandamanaji Ijumaa waliyavamia makumbusho ya vitu vya kale mjini Algiers na Televisheni ya Serikali imeripoti juu ya kuzuka kwa moto ndani ya jengo yaliyopo makumbusho hayo na baadhi ya vitu vya kale.

Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya Usalama wa Taifa, watu wapatao 195 wamezuiwa na maOfisa wa polisi 112 walijeruhiwa kwenye maandamano hayo.

Rais Bouteflika, ameonya juu ya kutokea machafuko na ameyalaumu makundi kutoka nje ambayo amesema yanataka kuyatumia maandamno hayo kuvuruga amani nchini Algeria.

Bouteflika alinusurika vuguvugu la kupinga Serikali lililoanzia nchi jirani ya Tunisia mnamo mwaka 2010.

Wakati huo, Serikali yake ilifaulu kuyazima maandamano ya kuunga mkono demokrasia kwa kutoa ahadi za kufanya mageuzi na kuongeza mishahara kwa kutumia mapato ya nchi yanayotokana na mafuta na gesi.

Katika miaka ya karibuni, uchumi wa Algeria umedorora kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa hali ambayo pia imesababisha kupungua kwa ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa wananchi.