Wananchi Misri kuupigia kura muda wa Rais

Muktasari:

  • Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya utawala wamesema kwamba uamuzi wa Bunge kumtaka kiongozi wa nchi hiyo aongezewe muda huenda ukasababisha vurugu

Cairo, Misri. Raia wa Misri, Jumatatu watapigia kura ya mabadiliko yaliyofanywa na wabunge kumruhusu Rais Abdel Fattah al-Sisi kuwa madarakani hadi mwaka 2030.

Wabunge hao pia wanataka jeshi la nchi hiyo lipewe nafasi kubwa ya kuamua mustakabali wa hali ya kisiasa kwenye taifa hilo.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanaonya kuwa huenda mabadiliko hayo yakaitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo mwingine wa kisiasa licha ya kuwa jeshi bado linaungwa mkono.

Mbali na mabadiliko hayo, wabunge wamemuongezea Rais Al Sisi madaraka ya kudhibiti Idara ya Mahakama lakini pia jeshi litaendelea kuwa na nguvu katika siasa za nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini.

Rais Al Sisi, ambaye alichaguliwa mwaka  2018, muhula wake wa miaka sita ulitarajiwa kumalizika  2024, lakini iwapo mabadiliko hayo yataungwa mkono, anaweza kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka sita.

Al Sisi aliingia madarakani mwaka 2013, baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi kumpindua rais aliyekuwa amechaguliwa wakati huo, Mohamed Morsi.