Wapinzani wasema wanajua sababu ya jeshi kutaka kuipindua Serikali Gabon

Tuesday January 8 2019

 

Libreville, Gabon. Baada ya Jeshi la Gabon kufanya jaribio la kuipindua Serikali, wapinzani wa nchi hiyo wamesema kwamba wanafahamu kwa kina chanzo cha uamuzi wa jeshi hilo.

Jean Ping ambaye ni msemaji wa kinara wa upinzani nchini humo, Laurence Ndong, alisema  wao wameelewa kwa nini wanajeshi hao walijaribu kuipindua Serikali.

Hata hivyo msemaji huyo hakutaka kueleza sababu za uamuzi wa jeshi hilo ambalo lilifanya jaribio hilo juzi wakati  Rais Ali Bongo wa nchi hiyo akiwa nchini Morocco kwa matibabu.

Rais huyo  anapatiwa matibabu  kwa zaidi ya miezi miwili sasa tangu aanze kuugua akiwa nchini Saudi Arabia.

Hata hivyo, vyombo vya usalama nchini Gabon vimefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi hayo na kiongozi wa wanajeshi walioshiriki jaribio hilo amekamatwa na wengine wawili wameuawa.

Jaribio hili limewaibua viongozi wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa ambao wamesema hakuna demokrasia itakayopatikana kwa nguvu ya kijeshi au kupitia mapinduzi.

Hali ya utulivu imerejea nchini humo huku usalama ukiwa umeimarishwa kwenye maeneo mengi ya nchi kwa mujibu wa msemaji wa Serikali ya Gabon, Guy Betrand Mapangou.

Balozi wa Gabon nchini Ufaransa, Flavien Enongoue, alisema  uchunguzi tayari umeanza kubaini wanajeshi zaidi waliohusika.

Msemaji wa Serikali ya Gabon alisema maofisa wa jeshi wote isipokuwa mmoja tu kati ya walioshiriki jaribio la kupindua Serikali mapema Jumatatu wamekamatwa.

“Wanne wamekamatwa na mmoja amekimbia,” alisema  Mapangou.

Maofisa wa jeshi walikiteka kituo cha radio cha taifa kinachomilikiwa na Serikali, Jumatatu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Libreville.

Wanajeshi hao walieleza dhamiri yao ya kuunda baraza la kitaifa la kuendesha nchi hiyo.

Luteni Kelly Ondo Obiang alisema katika radio hiyo kuwa hotuba ya Rais Bongo aliyoitoa kupitia radio ya nchi hiyo ilithibitisha wasiwasi uliopo juu ya uwezo wa Rais katika kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni alipeleka wafanyakazi wa Jeshi la Marekani huko Gabon kwa sababu ya kuwepo wasiwasi wa kutokea machafuko katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Advertisement