Wasemaji ANC kuachia ngazi kwa kashfa za ngono

Wednesday February 27 2019

Chama kinachoongoza Afrika Kusini cha ANC jana kimesema kuwa wasemaji wake wawili wataachia ngazi, ikiwa ni miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi kutokana na makosa tofauti ya tuhuma za ngono.
Mwezi Desemba, msemaji wa ANC, Pule Mabe alituhumiwa na msaidizi wake wa zamani kwa kutumia matusi na kumkata mshahara wake wa mwezi hadi kufikia dola 1.08 baada ya kukataa kufanya naye mapenzi.
Wiki iliyopita, tuhuma za kubaka zilitolewa dhidi ya Zizi Kodwa, ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya msemaji wakati shauri la Mabe likichunguzwa.
Akizungumza akiwa makao makuu ya chama hicho jijini Johannesburg, katibu mkuu wa ANC, Ace Magashule aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanachama hao waandamizi wameamua kujiuzulu nafasi zao wakati madai hayo yakichunguzwa.
"Kwa hiyo ANC imekubali maombi yao ya kujiuzulu kwa hiyari yao wakati wakishughulikia suala hilo," chama kilisema katika taarifa yake.
"ANC ina nia ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia kokote unakotokea na inachukulia tuhuma dhidi ya mtu yeyote kwa uzito unaotakiwa."
Ingawa uchunguzi wa ndani ulionyesha Mabe hana hatia mapema mwezi huu, inasadikiwa kuwa aliyemtimua amefikisha suala hilo polisi.
Wote wawili wamekana kufanya kosa lolote lakini chama hicho si mgeni kwa matukio kama hayo ya kashfa za ngono.
kabla ya kuingia madarakani, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alifikishwa mahakamani mwaka 2006 kwa tuhuma za kubaka, ambazo ziliudhi wananchi wengi.
Mabe na Kodwa, ambao walikuwa na nguvu kwenye chama enzi za Nelson Mandela, wataendelea kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya ANC, chombo kinachofanya maamuzi ya shughuli za kila siku.

Advertisement