VIDEO: Waziri Ndalichako amemvua madaraka mkuu wa Chuo cha ualimu Mpwapwa

Muktasari:

  • Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amemvua madaraka mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa jijini Dodoma, Benjamin Mwilapa

Morogoro. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amemvua madaraka mkuu wa chuo cha ualimu Mpwapwa jijini Dodoma, Benjamin Mwilapa.

Amevuliwa madaraka hayo kwa tuhuma za kuhusika na ubadhilifu wa zaidi ya Sh1.5bilioni za miradi ya ukarabati wa madarasa na miundombinu ya chuo cha ualimu Ilonga.

Kabla ya kuhamishiwa katika chuo cha ualimu mpwapwa, Mwilapa alikuwa mkuu wa chuo cha ualimu Ilonga na pia alikuwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi.

Baada ya tuhuma hizo Profesa Ndalichako ameagiza arudi Ilonga kujibu tuhuma hizo.

Akizungumza leo Jumanne Februari 12, 2019 Ndalichako amesema alibaini ubadhilifu huo mara baada ya kukagua miradi hiyo iliyojengwa chini ya kiwango huku ofisa ugavi, Ally Masanja na mhasibu wa chuo,  Godlove Yohna nao akiwasimamisha kazi kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi.

Akikagua miradi hiyo Profesa Ndalichako amesema  thamani ya fedha iliyotumika hailingani na ubora wa miradi hiyo, akibainisha kuwa kuna ubabaishaji mkubwa umefanywa.

Katika miradi hiyo ya ukarabati wa madarasa, mabweni na miundombinu ya maji, waziri huyo alishuhudia nyufa kwenye sakafu, milango na madirisha iliyotengenezwa kwa mbao zisizokuwa ubora huku nyingine zikiwa zimeshatumika.

Pia alionyesha kukerwa na usimamizi mbovu uliofanywa na wahandisi washauri wa miradi hiyo kutoka chuo cha sayansi na teknolojia Mbeya na kumtaka mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Msambichaka kufika haraka ili kuona ubadhilifu huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa,  Adamu Mgoyi ameahidi kuchunguza ubadhirifu huo, huku akiomba ofisi yake kushirikishwa katika miradi mikubwa ya Serikali ili aweze kufuatilia.

Awali mjumbe wa kamati ya ununuzi wa vifaa vya mradi huo,  John Mwiru amesema mara kadhaa kamati hiyo imekuwa ikishinikizwa kununua baadhi ya vifaa bila ya kushirikishwa kwenye vikao vya kupitisha manunuzi.