Wosia alioacha mtendaji mkuu wa Safaricom

Nairobi. Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Radio Africa Group, Patrick Quarcoo, amefichua kuwa aliyekuwa mtendaji mkuu wa Safaricom, Bob Collymore aliwaomba marafiki zake wasimame na mkewe, Wambui Kamiru, baada ya yeye kuipa dunia kisogo.

Quarcoo alikumbuka namna Collymore alivyotania kwenye kikao chao cha mwisho kwamba baada ya kufariki dunia baadaye atarejea kama pepo.

“Sijui kuhusu jambo hili la mbinguni na duniani, lakini natumaini kwa dhati kwamba kuna uhai baada ya kifo,” alisema Quarcoo akimnukuu Collymore.

Quarcoo alisema walipomuuliza maana ya kauli yake hiyo aliwajibu kwa utani: Iwapo kuna mapepo, nitarejea na kufungua pazia, na wakati wa sherehe za siku ya kuzaliwa kwa watoto wangu mtakapowasha mishumaa nitakuja na kuwasaidia kuipuliza.”

Mzaliwa huyo wa Guyana alikuwa akizungumza na kundi la marafiki zake ambao ni pamoja na Quarcoo, Jeff Koinange, Bharat Thakrar, Nic Hailey, Peter Kenneth na Alykhan Satchu.

Katika wosia ulioibua hisia, Quarcoo alisimulia ujumbe wa mwisho wa kigogo huyo kuhusiana na mkewe mpendwa.

“Nikijaliwa kuishi kwa siku tatu zaidi nitakuwa na bahati. Dumisheni umoja, simameni na mke wangu Wambui nikiondoka,”  alinukuliwa Collymore katika siku zake za mwisho duniani.

Quarcoo alimkumbuka marehemu Collymore kama mtu “aliyewabadilisha marafiki zake wote. Alitufanya kuwa na utu zaidi, wenye moyo safi zaidi kama yeye binafsi na kuwa rahisi kufunguka.” Collymore aliaga dunia Julai 1, 2019 kutokana ugonjwa wa saratani.