Zimbabwe kuwafidia walionyang’anywa mashamba

Muktasari:

  • Ni wale wazungu waliokuwa wanamiliki mashamba makubwa na kunyang’anywa na Serikali iliyokuwa madarakani

Harare, Zimbabwe. Kuanzia mwezi ujao Serikali ya Zimbabwe itaanza kufidia maelfu ya wakulima wazungu ambao walinyang'anywa mashamba kwa nguvu wakati wa mageuzi ya sera ya umiliki wa mashamba iliyoanzishwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe mwishoni mwa miaka ya 2000.

Mugabe aliwataka wakulima wazungu waliobakia  nchini humo kuondoka na kuwaachia mashamba wazalendo wa nchi hiyo.

"Hatuwataki wakulima wazungu kumiliki mashamba yetu, lazima waondoke,'' Mugabe aliwaambia wafuasi wake katika mkutano wa hadhara.

Mrithi wake, Rais Emmerson Mnagagwa ameapa kuinua kilimo ikiwa ni moja ya malengo yake makuu katika mageuzi ya kiuchumi. Pia aliwatolewa wito wawekezaji wa kimataifa kuchangia katika kuendeleza uchumi wa nchi hiyo ambao uko hatarini.

Mageuzi ya sera ya umiliki wa mashamba yaliyozinduliwa na  Mugabe katika miaka ya 2000 yalisababisha athari kubwa za kiuchumi. Kwa kuwanyng'anya wakulima 4,000 mashamba yao, Rais Mugabe alitaka kurekebisha haki ya kijamii iliyotokana na ukoloni. Lakini hatua yake kuhusu mageuzi katika sekta hiyo ilizua sintofahamu na kusababisha  mdororo wa kiuchumi.

Wakosoaji wa Rais Mugabe wanasema kuwa sera yake ya kutaka umiliki mashamba yote yanayomilikiwa na wazungu ndiio ilisababisha kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo kati ya mwaka 2000-2009.