Zuma adai tuhuma za rushwa dhidi yake zilipikwa na shirika la upelelezi la kigeni

Muktasari:

Rais Jacob Zuma ameiambia mahakama nchini humo kuwa tuhuma zinazomkabili ni njama zilizokuwa na lengo la kumuondoa katika ulimwengu wa siasa.

Durban, Afrika Kusini. Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ameiambia mahakama nchini humo kuwa tuhuma za rushwa dhidi yake ni njama zilizokuwa na lengo la kumuondoa katika ulimwengu wa siasa.

Rais Zuma amesema hayo leo Jumatatu Julai 15 alipofika kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Juu kwa ajili ya utetezi dhidi ya mashtaka ya rushwa na ufisadi yanayomkabili.

Kutokana na tuhuma hizo Februari mwaka 2018, Rais Zuma alijiuzulu urais na nafasi hiyo kuchukuliwa na naibu wake, Cyril Ramaphosa.

Zuma anakabiliwa na mashtaka ya rushwa, udanganyifu na kujitajirisha kinyume cha sheria kwa kufanya biashara ya mauzo ya silaha akiwa makamu wa rais wa nchi hiyo.

Alichokisema Zuma mahakamani

Rais Zuma ambaye jana alionekana ametulia alidai shirika la upelelezi la kigeni ambalo hata hivyo, hakulitaja lipo nyuma ya sakata hilo kwa lengo la kumtoa katika ofisi.

“Nimejihakikishia kwamba nilituhumiwa kuwa mimi ni mfalme wa rushwa,” alisema Zumba mbele ya Jaji Ray Zondo anayesikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, Zuma alidai kuwa alipewa majina yote ya watu waliopanga njama hizo ingawa hakufuatilia zaidi kuhusu sakata hilo.

"Je, niliuza mlima wa Table mountain? Je, niliuza Jiji la Johannesburg? Alihoji Zuma mahakamani hapo.

Tuhuma za Zuma

Rais Zuma anashutumiwa kupokea rushwa kutoka katika kampuni ya Ufaransa ya Thales ili kuipa mkataba wa mauzo ya silaha ulioafikiwa mwaka 1999.

Kiongozi huyo ambaye anatuhumiwa kuwa na uhusiano na familia ya Gupta anadaiwa kushawishi baraza la mawaziri kumpatia mkataba huo wenye faida kubwa. 

Pia, kiongozi huyo anatuhumiwa kupokea rushwa katika kampuni ya vifaa ya Bosasa iliyokuwa ikiendeshwa na familia ya Watson.