Kinachotekelezwa ni mpango wa Taifa sio ilani ya CCM - Chadema

Wafuasi wa Chadema wakizunguka mitaani na pikipiki wakati wa kampeni za kumnadi mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya chama hicho walipokuwa wakielekea mkutano wa kampeni uliofanyika Kivule jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Dk Mashinji alisema hayo juzi baada ya mkutano wa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya chama hicho, Asia Msangi uliofanyika kwenye Kata ya Majohe, Mtaa wa Kichangani.

Dar es salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema kitendo cha CCM kujinadi kuwa kinatekeleza miradi ya maendeleo kupitia ilani yake wakati ni mpango wa maendeleo wa Taifa ni upotoshaji.

Dk Mashinji alisema hayo juzi baada ya mkutano wa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya chama hicho, Asia Msangi uliofanyika kwenye Kata ya Majohe, Mtaa wa Kichangani.

Badala yake, Dk Mashinji alisema ilani ya chama hutumika wakati wa uchaguzi tu ili kuwapa mwelekeo wananchi wachague chama gani na kwamba baada ya uchaguzi, bunge la kwanza hupitisha mpango wa maendeleo wa Taifa ambao umeainisha kila kitu na ndiyo unaotekelezwa kwa kipindi kilichopangwa.

Alisema baada ya mpango huo, Serikali iliyopo madarakani ndiyo inayokuwa na jukumu la kuutekeleza.

“Kama kuna chama kinatekeleza ilani ya chama chake kuleta maendeleo, basi tusiyategemee na kitakuwa kinavunja sheria ya nchi na ya fedha kwa sababu hizi zote huendana na mpango wa maendeleo wa Taifa,” alisema Dk Mashinji.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wameendelea kuwadanganya wananchi kuwa watawapa kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kujenga hospitali na shule na kusahau kuwa utoaji fedha za nchi si wa mtu mmoja, bali ni utekekezaji wa yaliyomo kwenye mpango wa maendeleo wa Taifa ambao umepitishwa na Bunge.

“Wananchi wapuuzie hizi tambo, hakuna ilani inayotekelezwa nje ya mpango wa maendeleo wa Taifa na kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Sheria ya Fedha,” alisema Dk Mashinji.

Ulinzi wa amani

Mbali ya kuzungumzia ilani za uchaguzi, Dk Mashinji pia alisema upinzani hauko tayari kuona amani ya nchi ikivunjika kwa sababu tu ya uroho wa madaraka wa watu wachache.

Alisema katika kuhakikisha Amani inalindwa, viongozi wa chama chake wameendelea kuihubiri hata pale wanapokumbwa na vikwazo katika chaguzi ndogo zinazoendelea nchini.

Alisema hivi sasa kuna vitendo vingi vya uvunjifu wa sheria vinavyofanyika kwenye maeneo yaliyo na uchaguzi mdogo ikiwamo utangazaji wa matokeo na upokeaji wa fomu kwenye ambavyo alidai sio wa haki.

“Lakini sisi tumeendelea kuvumilia, tungekuwa wapuuzi na wajinga tungeshavunja amani ya nchi kwa kuwashirikisha wananchi ambao bado wanatuunga mkono. Lakini hatupo tayari kuona amani ya nchi inavunjika kwa sababu ya watu wa chache, ndiyo maana tumekuwa tukihubiri amani licha ya kufanyiwa dhuluma za wazi,” alisema Dk Mashinji.

Hata hivyo, alisema hawatakuwa tayari kunyanyasika na kwamba wataendelea kukemea vitendo viovu ili wananchi wafahamu.

Kauli ya Mnyika

Mbunge wa Kibamba John Mnyika alisema licha ya ‘figisufigisu’ wanazofanyiwa, upinzani hauwezi kufa na badala yake unazidi kuwa imara na kuwataka wananchi wa Ukonga kuwa na moyo wa mabadiliko ili wajiletee maendeleo.

Alisema katika maeneo yote wanayopita kufanya kampeni, wananchi wanajitokeza kwa wingi na wanawaunga mkono.

“Jana nimejaribu kwa dakika chache kufanya harambee ya kuchangia mafuta kwa chama, jambo ambalo wananchi wa chini kabisa walianza kuchangia kwa kutoa Sh500 na Sh100 na baada ya muda mfupi tukakusanya Sh115,000. Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani watu wapo tayari kwa mabadiliko.” alisema Mnyika.

Hata hivyo, Mnyika alidai kuwa kumekuwa na hujuma zikifanyika kwenye maeneo hayo ikiwamo kununuliwa kwa shahada za kupigia.