Wanafunzi wa kike watumia mtandao kujiuza

Sunday February 3 2013

 

By Waandishi Wetu

PENGINE haya tunaweza kuyaweka kwenye kundi la madhara yatokanayo na utandawazi. Mitandao ya kijamii ipo inayowasaidia wanafunzi katika masomo yao na kazi, lakini wengine wanatumia mitandao hiyo visivyo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa matumizi mabaya ya teknolojia hasa mitandao ya kijamii yamechochea ongezeko la uhalifu, ubakaji, matumizi ya dawa za kulevya na zaidi biashara ya ukahaba vyuoni.

Mitandao ya ‘Facebook’, ‘Twitter’, ‘BBM’, ‘Instagram’ inafahamika kwa namna inavyoweza kuwaunganisha watu kutokana na urahisi wake katika kuitumia.

Mwananchi Jumapili limebaini kuwa katika mitandao hiyo makundi mbalimbali yameanzishwa yakiwa na malengo tofauti.

Baadhi wameanzisha makundi kwa lengo la kujenga mitandao ya kibishara, kidini, michezo, burudani, vichekesho na mengine ambayo mara nyingi huwa wazi na yeyote anaweza kujiunga na kuona kinachoendelea ndani.

Mbali na hayo ndani ya mtandao wa ‘Facebook na ‘BBM’ yapo makundi yanayoendesha biashara ya ukahaba, yakiwahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Advertisement

Uchunguzi umebaini kuwa wanafunzi hao wanaofanya biashara ya ukahaba kwa kutumia mitandao wameweka picha na namba kwa ajili ya mawasiliano kwa mteja atakayekubaliana na bei waliyoweka.

Baadhi ya wanafunzi hao wanatumia mtandao wa ‘University Tanzania  Jokes’, ‘Jicho la Mvulana Liko Fasta Kuliko Google’, ‘Benki ya Utamu Tanzania’ na nyingine katika kufanikisha biashara hiyo ya ngono.

Ukiingia katika mitandao ya Facebook, Twitter, BBM, Instagram, utabaini kuwapo kwa makundi yaliyoundwa kutengeneza mitandao ya ngono, ambayo huweka pia namba za  simu za wahusika, zikiambatana na picha, ambao ikiwa utaangalia picha na kuvutiwa, unaweza ukapiga simu husika kuzungumza naye kwa kufanya mapatano kabla ya kukubaliana.

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa mwanamume anaweza kumpata msichana kutoka chuo kikuu chochote nchini anayefanya biashara ya ukahaba kupitia mitandao hiyo.

Baadhi ya vyuo wanavyotoka wasichana wanaofanya biashara hiyo na kujitangaza kwenye mitandao ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Kwa nyakati tofauti, waandishi wa gazeti hili walitembelea makundi yanayojinadi kufanya biashara hiyo pamoja na kufanya mawasiliano na wasichana watatu ambao waliweka picha na namba zao kwenye mtandao.

Wasichana hao walijitambulisha kwa majina, vyuo na vitivo wanavyosoma na baada ya kuwafuatilia kwa kuweka ahadi za kimapenzi ilithibitika kuwa wanafanya biashara ya ukahaba huku wakiwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Mmoja wa wasichana hao alijitambulisha kwa jina la Bianca (sio jina lake halisi), ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baada ya mwandishi kufanya naye mawasiliano walikubaliana kukutana eneo la Udasa na muda wa ahadi ulipofika, mwandishi alifika eneo hilo na kukutana na binti huyo ambaye aliiona picha yake na namba ya simu kwenye mtandao, tofauti na alivyodhani awali kuwa huenda wasichana hao wanatumia picha za watu wengine kujinadi.

Kutokana na lengo la msichana kuwa ni biashara ya ngono, mwandishi wa gazeti hili alilazimika kumpeleka binti huyo katika hoteli moja maarufu jijini, akimweleza kuwa inabidi wanywe pombe kwanza kabla ya kwenda chumbani kwa makubaliano ya kumlipa Sh50,000.

Binti huyo alikabidhiwa fedha hizo ili kumwaminisha uhalisia wa kuwapo hitaji na muda wa kwenda naye chumbani ulipofika waliongozana lakini mwandishi akatoroka  njiani akiwa amethibitisha kuwapo kwa tabia hiyo.

Gazeti hili lilimfuatilia mwanafunzi mwingine ambaye alijitambulisha kuwa anasoma katika Chuo cha Ustawi wa Jamii, ambaye kama ilivyokuwa kwa wa kwanza, hakupata taabu kujieleza.

Baada ya mwandishi kueleza alipoipata namba yake mazungumzo yao yalikuwa hivi:
Binti aliuliza: “...Kwa hiyo, uko wapi?”
Mwandishi alijibu:  “Nipo Ubungo.”
Binti akauliza tena: “Unaweza kuja Ustawi?”

Baada ya mawasiliano hayo mwandishi aliambiwa binti huyo kuwa anaweza kumfuata chuoni hapo.

Mwandishi wa gazeti hili alifika maeneo ya Kijitonyama jirani na kilipo chuo hicho, na kumpigia simu binti huyo, ambaye aliipokea na safari hii alimwambia mwandishi kuwa ikiwezekana aje na rafiki yake.

Ilichukua nusu saa kwa wasichana hao kufika katika baa, ambayo mwandishi alikaa kuwasubiri, mara walitokea wasichana hao wakiwa wachangamfu, warembo waliovalia mavazi ya kisasa, yaliyoacha sehemu kubwa ya miili yao wazi.

Muda wa dakika saba walizokaa zilitosha kuwafanya wazoeane na mwandishi kama vile waliwahi kukutana miaka mingi ya nyuma, stori, vinywaji na mambo yalifanyika  kama ilivyokuwa Udasa.

Mwananchi Jumapili liliendelea na uchunguzi wake kwa wasichana wengine ambao wameweka picha zao katika mitandao hiyo wakijiuza, ambapo walipopigiwa simu walijibu na kufika katika maeneo waliyokubaliana.

Gazeti hili liliwasiliana na wasichana zaidi ya 10 kutoka katika vyuo tofauti jijini na wote walikiri kuwa wapo katika biashara wakieleza kuwa mteja akipatikana wanaweza kukubaliana malipo.

Wasichana hao ni tone kati ya mamia ya wanafunzi wa vyuo, ambao hivi sasa wamebuni njia hiyo baada ya kuona ule mtindo wa kujiuza nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali kuwa umeanza kupitwa na wakati.

Baadhi ya wasichana wanaofanya biashara hiyo hasa mkoani Dodoma, wamekuwa wakiwatumia mawakala ambao huwapa namba za simu na pindi anapotokea mteja, huunganishwa na kiongozi wa kikundi hicho kabla ya kupata aina ya msichana anayetaka.

Hata hivyo mteja asiporidhika na msichana aliyeletewa, hutafutiwa mwingine, huku pia wasichana husika wakitofautiana mahitaji kabla ya kufanya nao ngono.

Wapo wanaoweka masharti ya kunyweshwa pombe kwanza, kupelekwa disko au kwenye muziki pamoja na wanaokwenda kwa matakwa ya mteja moja kwa moja.

Wanafunzi wazungumza
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili baadhi ya wanafunzi walikiri kuwa katika vyuo kuna wasichana wanaojiuza, ingawa walisema kuwa, hawajui kama wamefikia hatua ya kuweka picha katika mitandao na namba za simu.

Mwanafunzi Aisha Idd wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), alisema kuwa biashara ya ukahaba inafanyika, lakini hafahamu kama wanatumia mitandao kujitangaza.

“Sijawahi kufikiria kama wanaweza kufika mbali kiasi hiki, sijui kama wanajiuza kwenye mitandao, lakini hii inaonyesha kuwa tunakoelekea ni kubaya zaidi kwani hawa ndio watu wanaotegemewa katika ujenzi wa taifa,” anasema Aisha na kuongeza:

“Ninafikiri Serikali inapaswa kuliangalia hili, yaani wasomi ndiyo wanaoongoza kwa kufanya mambo machafu, hii  ni aibu na inaweza kuitia doa sekta nzima ya elimu ionekane haina maana kama msomi wa chuo kikuu anaweza kufanya upuuzi huu.”

Naye John Mkongo alisema kuwa hashangai kusikia kuwa wanafunzi hao wametafuta njia nyingine ya kutafutia wateja kwa kuwa wanaweza kufanya chochote ili wapate pesa za kufanyia starehe.

“Hii inawezekana kabisa kwani hawa dada zetu wamefikia kufanya mambo ya ajabu kama vile wamepata wazimu, ili kupata pesa wanaweza kukubali kufanya chochote, najua siku za usoni tutaendelea kusikia mambo ya ajabu zaidi kwani hawa wenzetu wamejitoa mhanga,” anasema Mkongo.

Anaongeza kuwa kinachowafanya wasichana hao kujiingiza katika biashara ya ukahaba ni tamaa, akitoa mfano baadhi ya wasichana ambao hawajihusishi kabisa na mambo hayo.

“Mimi ninaona kinachowagharimu hawa dada zetu ni tamaa tu, huku wengine wakiponzwa na ulimbukeni wa kuvamia mambo, ambayo wameanza kuyaona baada ya kuingia chuoni hasa kupenda vitu vya gharama kama vile simu, nguo, manukato na magari,”anasema Mkongo.

Wakuu wa vyuo wanena
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Tolly Mbwete anasema hali hiyo inatokana na kukua kwa utandawazi.

“Ni wakati sasa kwa wizara inayohusika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ) kuhakikisha inafuatilia jambo hili na kuchukua hatua stahiki,” anasema Profesa Mbwete na kuongeza:
“Elimu nayo inatakiwa kutolewa kwa watumiaji ili kutokuathiri dhamira ya kukua kwa utandawazi, jamii nzima ielimishwe kuhusu matumizi sahihi ya mitandao hiyo.”

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula, anasema kuwa hana taarifa za kuwapo kwa makundi hayo lakini akabainisha kuwa unatakiwa kuwapo kwa utafiti ili kujiridhisha kama ni kweli hao wanaofanya hivyo ni wanafunzi wa vyuo.

Anasema kama yapo ni wakati sasa wa kuhakikisha wanakemewa kwani kuna baadhi ya wasichana wanatumia mitandao kujitambulisha kuwa ni wanafunzi wa vyuo, wakati siyo wanafunzi.

“Hapa Dodoma katika kipindi cha Bunge wanawake wanaojiuza huwa wengi kila unayemuuliza atakwambia anasoma chuo, lakini ukimuuliza kozi gani atakwambia bado sijapangiwa hivyo hii ni hatari,” anasema Profesa Kikula.

Wazazi wasikitika
Mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, Florence Baltazar anasema vitendo hivyo vinatokea kwa sababu ya kuiga mambo ya nchi za nje.

Baltazari anasema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania  (TCRA), inatakiwa kuhakikisha inafuatilia mitandao hiyo ikibidi kuifunga kabisa.
Zubeda Hamza anasema vijana wa siku hizi hawajitambui hususan wasichana ambao wamekuwa hawapo makini na utu wao.

“Kweli kama msichana anajitambua hawezi kutongozwa katika mtandao na kukubali haraka au kujinadi hivyo wasichana wanatakiwa kutambua utu wao,”anasema na kuongeza:

“TCRA inatakiwa kuwa inafanya mapitio ya mitandao yote ili ile inayokiuka taratibu waweze kuifungia.”

Kwa upande wake Charles Mashiri anasema kuwa wasichana wa siku hizi wamekuwa hawashikiki, hasa wanapofika vyuoni na kwamba hawataki kukaripiwa au kuonywa.

“Akiwa nyumbani anakuwa mtaratibu lakini akitega mgongo kutoka kutoka nyumbani anaanza tena ujinga wake, hivyo kama vitendo hivyo vipo basi Serikali inatakiwa kufuatilia na kuchukua hatua zaidi,”anasema.

Advertisement