Kibanda kubakia hospitali siku 40

Tuesday March 12 2013

Rais Jakaya Kikwete alipomtembelea Mwenyekiti

Rais Jakaya Kikwete alipomtembelea Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Absalom Kibanda. 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Absalom Kibanda atabaki kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini anakotibiwa kwa siku 40 kuanzia leo.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Tef, Neville Meena imesema madaktari wamemweleza Kibanda kuwa baada ya siku hizo ndipo watakapomfanyia upasuaji kwa mara ya pili.

Meena alisema kuwa operesheni hiyo itakuwa ya kumwekea jicho bandia baada ya kuondolewa lile lililoharibika kutokana na kushambuliwa na watu wasiojulikana hivi karibuni.

Meena alisema hali ya kiongozi huyo wa wahariri inaendelea vyema na katika kuthibitisha hilo alisema kwa mara ya kwanza tangu alazwe hospitalini hapo alizungumza naye moja kwa moja kwa simu.

“Aliniambia kuwa ana nafuu kubwa licha ya kwamba hajawa na uwezo wa kuzungumza kama mwanzo. Bado hajaamka kwa kuwa anasikia maumivu. Ila ametamka kuwa anaendelea vizuri. Amesema kwa ujumla hali yake inaridhisha kwa sasa tofauti na mwanzo,” alisema Meena.

Meena aliendelea kueleza kuwa Kibanda anaendelea na matumizi ya dawa baada ya upasuaji aliofanyiwa Jumamosi iliyopita.

Advertisement