Utekaji watu Tanzania: Baada ya Kibanda nani atafuata-2?

Monday March 18 2013

 

Padri auawa Zanzibar kwa risasi
Tukio lingine ambalo lilishtua wengi ni la kuawa kwa Padri Evarist Mushi, Paroko wa Parokia ya Minara Miwili , Zanzibar. Yeye, aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na kufa papo hapo na watu wasiojulikana asubuhi akielekea kanisani.

Msemaji wa Polisi Zanzibar, Inspekta Mohamed Mhina alithibitisha tukio hilo huku akisisitiza  kuwa uchunguzi wa kina zaidi ungefanyika kuhakikisha waliofanya hilo wanachukuliwa hatua.

Mwingine apigwa risasi
Awali, Kabla ya kuuawa padri Mushi, padri mwingine, Ambrose Mkenda naye alipigwa risasi na watu wasiofahamika kwenye lango  la nyumba yake maeneo ya Kitomondo mjini Zanzibar, ambako ndiko makazi yake yalipo akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha pekee yake.

Hali yake siyo nzuri kwani risasi aliyopigwa imemdhuru maeneo ya mdomoni na hadi sasa bado hajaweza kuwa imara. Waliompiga risasi padri huyo inasemekana ni watu waliokuwa kwenye pikipiki, ambao walimvamia akisubiria afunguliwe geti kuingia nyumbani kwake.

Katibu wa Mufti amwagiwa tindikali
Pia Zanzibar ilikumbwa na tukio la linalofanana na matukio hayo kwani kiongozi mwingine wa dini aliingia kwenye msukosuko.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, alimwagiwa tindikali na watu wasiyojulikana huko Magogoni Msumbiji Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Yussuf Ilembo, alisema Sheikh Soraga alimwagiwa tindikali majira ya alfajiri alipokuwa akifanya mazoezi ya viungo.

Ni kwamba wakati akifanya mazoezi, alimuona mtu akifanya mazoezi akielekea mbele yake na baada ya kukutana uso kwa uso alimmwagia tindikali na kumjeruhi sehemu za usoni na kifua kabla ya mtu huyo kutoweka.

Dk Stephen Ulimboka
Kiongozi   wa jumuiya ya Madaktari  Tanzania, Dk Stephen Ulimboka, saa sita usiku alitekwa, kupigwa na watu watatu wenye silaha na kisha kutupwa maeneo ya mabwepande ambapo aliokotwa na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) jijini Dar es Salaam.

Wengi wanahoji sababu ya kutekwa Dk Ulimboka, hasa kutokana na ukweli kwamba si mfanyabiashara…Nani alimteka kwa lipi? Ni swali lisilo na jibu.

Dk Ulimboka aliwahi kuwaambia waandishi wa habari na baadaye akasisitiza kauli hiyo kupitia wanasheria wake, Oktoba 2012, kuwa aliyehusika na mipango ya kutekwa na kuteswa kwake ni Ofisa wa Ikulu. Kama ni kweli, je, ofisa huyo alitumwa au alijituma ? Na je, aliwahi kuhojiwa polisi ili Ikulu ijisafishe kutoka katika madai haya ya Dk Ulimboka?

Waandishi wa habari wauawa
Baadhi ya waandishi wa habari waliouawa katika mazingira ya utata ni pamoja na wa  Kituo cha Redio Kwizera wilayani Kakonko mkoani Kigoma, Issa Ngumba (45)  ambaye aliuawa kwa kunyongwa na kisha kupigwa risasi mkono wa kushoto.

Mwili wake ulipatikana katika pori la Mlima Kajuluheta Kijiji cha Muhange, wilayani humo asubuhi baada ya wananchi kufanya msako wa siku tatu mfululizo bila mafanikio.
Lakini, pia vitendo kama hivyo vinawakuta wenye ulemavu wa ngozi ambao wengi wameathirika , lakini waliohukumiwa kunyongwa tangu mwaka juzi mpaka sasa hawajanyongwa.

Richard Masatu auawa
Richard Masatu aliuawa Agosti 2011. Yeye, alikuwa Mkurugenzi wa gazeti la KASI MPYA, alifia Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure mjini Mwanza, akipatiwa matibabu. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa marehemu alifariki kutokana na majeraha ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.

Advertisement