Lissu apeleka kesi ya Lwakatare Mahakama Kuu

Thursday March 21 2013Tundu Lissu

Tundu Lissu 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi, Dar es Salaam.

Ibrahim Yamola, Mwananchi,
Dar es Salaam. Kesi inayowakabili Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura imechukua sura mpya kutokana mawakili wanaomtetea kiongozi huyo na mwenzake kupeleka suala hilo Mahakama Kuu.


Mmoja wa wanasheria watano wanaowatetea Lwakatare na mwenzake, Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari jana alisema hatua yao ya kwe nda Mahakama Kuu inatokana na ukweli kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameingilia uhuru wa Mahakama bila sababu za msingi.


Mbali na Lissu, mawakili wengine wanaomtetea Lwakatare ni Peter Kibatala, Mabere Marando, Abdallah Safari na Nyaronyo Kicheere.
Juzi, Lwakatare na Ludovick walifutiwa mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuachiwa huru, lakini hapohapo wakisha kukamatwa tena na kusomewa mashtaka yaleyale ya awali.


Juzi waliposomewa mashtaka upya, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za ugaidi, tofauti na Jumatatu waliposomewa mashtaka kwa mara ya kwanza ambapo walipewa fursa ya kukubali au kuyakana mashtaka hayo.


Kwa kuzingatia mazingira hayo, Lissu alisema katika maombi yao watakayoyawasilisha leo Mahakama Kuu, wataiomba iingilie kati mchakato huo ambao wanasema kimsingi unakiuka sheria.


Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema wameiomba Mahakama Kuu iyapitie majalada yote mawili ili haki iweze kutendekea.
“Tunapeleka Mahakama Kuu maombi ya hati ya dharura kuiomba kuyaitisha mafaili yote mawili ya Jumatatu na Jumatano ili kuyachunguza kuona haki kweli kama ilitendeka,”alisema Lissu na kuongeza:


“DPP ametumia vibaya madaraka aliyonayo kwa kuingilia uhuru wa Mahakama kwani haiwezekani akafuta mashtaka kisha kufungua tena bila kubadili shtaka hata moja ila kilichobadilika ni namba ya kesi tu hatujui ana maana gani.


Alisema: “Kitu kinachosikitisha kuona kuwa Serikali jana (juzi) ilikuwa inaumbuka kwa hili ni pale DPP anapowasilisha hati ya kufuta mashtaka isiyokuwa na anwani yake tena kipande cha karatasi. Hii kisheria siyo halali, alikuwa na lengo la kuibeba Serikali yake.”


Ilivyokuwa juzi
Washtakiwa hao waliachiwa huru juzi na Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru baada ya Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza kuwasilisha hati kutoka DPP, akiiomba Mahakama kuwaachia chini ya kifungu cha 91 (1).


Hakimu Mchauru alikubaliana na hati hiyo na kuwafutia mashtaka washtakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi namba 37 ya mwaka 2013, iliyokuwa na mashtaka manne yanayohusu vitendo vya ugaidi.

Advertisement