Mahakama yamkabidhi polisi mshirika wa Lwakatare

Wednesday March 27 2013

 

By James Magai na Tausi Ally, Mwananchi

Washtakiwa hao walikamatwa na polisi Machi 13, mwaka huu na kukaa rumande siku nne kabla ya kufikishwa kortini

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemkabidhi mshtakiwa wa pili katika kesi ya ugaidi, Ludovick Rwezaura Joseph, kwa  polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Joseph na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi mahakamani  wakidaiwa kula njama na kupanga mipango ya kumteka kisha kumdhuru kwa sumu, Dennis Msacky.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena mahakamani hapo Aprili 3, lakini habari zilizolifikia Mwananchi jana na kuthibitishwa na Mwendesha Mashtaka Mkuu Mahakama ya Kisutu, Tumaini Kweka zinasema juzi Mahakama hiyo ilitoa kibali cha kwenda kuhojiwa na polisi wa upelelezi wa kesi hiyo.

Wakili Kweka alisema baada ya Mahakama hiyo kutoa kibali, jana mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kisha akakabidhiwa polisi kwenda kuhojiwa zaidi.

Kutokana na uamuzi huo, mawakili wanaomtetea Lwakatare walikuja juu wakihoji sababu za hakimu kukubali maombi ya polisi wakati alikataa maombi yote siku waliposomewa mashtaka hayo.

“Tarehe 20, 2013 hakimu alikataa maombi yote ya pande zote  na kusema tupeleke Mahakama Kuu, Sasa imekuaje leo amewakubalia polisi kumchukua Ludovick na kukaa naye kwa siku mbili?” alihoji Tundu Lissu kwa niaba ya jopo la mawakili wanaomtetea Lwakatare na kuongeza:

“Polisi kumchukua na kuendelea kumhoji wakati walishamshtaki mahakamani, maana yake nini? Kwani polisi walipomshtaki hawakuwa na uhakika na makosa yake? Hii inanuka.”
Joseph na Lwakatare alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Machi 18, 2013 na kusomewa mashtaka hayo ambayo walikana.

Kutokana na hatua hiyo, jopo la mawakili wanaomtetea waliomba Mahakama iwape dhamana, jambo lililozua mvutano mkali baina yao na upande wa mashtaka, ulioongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza.

Hakimu Mchauru aliahirisha kesi hiyo na kuamuru kutoa uamuzi wa maombi hayo ya dhamana Machi 20, lakini tarehe hiyo kabla ya kusoma uamuzi huo, upande wa mashtaka uliwafutia mashtaka, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashtaki.

Kutokana na uamuzi wa DPP, Hakimu Mchauru hakuweza kuendelea badala yake aliamuru .washtakiwa hao kuachiwa huru. kutokana na hati hiyo.

Advertisement