Sifa kumi za mgombea urais wa CCM

Thursday May 14 2015

 

By Julias Mtatiro

Hivi karibuni nimesaidiana kimawazo na Watanzania wenzangu katika kufanya uchambuzi wa watu wanaotajwa au waliojitangaza kuwa watawania uteule wa urais kupitia CCM na nalishukuru gazeti hili kwa kukubali kuchapisha maoni yangu.

Haikuwa kazi nyepesi na namshukuru kila mmoja aliyetoa mchango wake wa mawazo na aliyefuatilia nilichoandika, lakini nawaomba radhi wale wote ambao hawakupenda nilivyoandika na hasa walioumizwa lakini mrejesho mkubwa niliopokea kutoka kwa jamii ni kuendelea kuifanya kazi hii kwa sababu ina tija kwa Taifa.

Kabla sijafunga ukurasa wa CCM na kuhamia kwa vyama vya upinzani niliona nimalizie na kidokezo cha mwisho cha uchambuzi mfupi wa fikra zangu juu ya nani anaweza kupitishwa na CCM kuwa mgombea na huenda Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa chama hicho kitashinda uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa kifupi nitajadili nanyi sifa kumi za mtu huyo kutokana na dalili na mwelekeo wa CCM, hali inayokabiliwa nayo hivi sasa na mpasuko unaoinyemelea.

1. Anayeelewana na kukubalika kwa Rais anayemaliza muda wake

Watu wengi niliozungumza nao wanaidharau sifa hii. Lakini bado naona kuwa CCM itaitumia kumpata mgombea. Watu wengi walijaribu kuniambia kuwa hata mwaka 1995, Benjamin Mkapa hakuwa chaguo la Ali Hassan Mwinyi na kwamba hata mwaka 2005, Jakaya Kikwete hakuwa chaguo la Mkapa na kwamba mwaka 2010 pia Kikwete hatapata chaguo lake.

Lakini nasisitiza kuwa nyakati zinabadilika sana na huenda CCM ikapitisha mgombea ambaye anaweza kuwa chaguo la Kikwete kwani Rais huyo anaifahamu CCM vizuri na amefanya mambo mengi katika siasa za chama hicho.

Hatari ya sifa hii

Chama kinapopitisha mgombea kwa sababu tu anafahamiana na kukubalika na kiongozi anayemaliza muda wake, huwa kuna hatari ya mpasuko mkubwa ikiwa wagombea wengine hawataridhishwa na upendeleo aliopewa mwenzao na hivyo wanaweza kufanya uamuzi wa kuondoka katika chama hicho.

2. Mchapakazi na mwadilifu lakini atakayekubali kusikiliza mahitaji na matakwa ya CCM

CCM inahitaji mgombea mchapakazi na mwadilifu ili kuziba baadhi ya mashimo yaliyoachwa na Serikali inayoondoka kwa haraka na lengo la kufanya hivi ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kukiamini na labda kukiunga mkono. Lakini CCM ya sasa bado inahitaji sana msaada wa Dola ili iendelee kuwa madarakani. Kuna wakati Rais Kikwete mwenyewe aliwahi kuwatamkia wana CCM kuwa wanafanya kazi kwa kutaka kusaidiwa na vyombo vya dola.

Hatari za sifa hii

Hatari iliyopo ni uendelezaji wa mambo yaleyale ambayo yamekikumba chama hicho kwa miongo kadhaa iliyopita. CCM inahitaji mtu mwadilifu, mchapakazi na ambaye atakataa kabisa kusikiliza matakwa ya chama chake ili ajenge uchumi imara wa nchi, nidhamu kwa watendaji wa Serikali na kusimamia maendeleo ya Taifa huku akiweka “Taifa Mbele na chama baadaye”. Mgombea wa CCM ambaye atakesha akitekeleza matakwa ya CCM hatakuwa tofauti na wenzake kadhaa waliopita.

3. Aliyekulia katika chama na anakijua vizuri

Naiona CCM ikimpitisha mgombea ambaye anakijua vizuri chama hicho na hasa aliyekulia ndani ya chama ikiamini kuwa atakuwa na uwezo mzuri wa kupambana na kuzikabili changamoto za kichama na za kiserikali huku akijua anachokifanya kwa masilahi ya chama na serikali.

Hatari ya sifa hii

Katika dunia ya leo ambayo vyama vinavyoendelea vinajaribu pia kutenganisha mamlaka ya kichama na kiserikali na hata kuwa na watu tofauti katika uongozi wa nchi na ule wa chama, sifa hii inajimaliza yenyewe.

Kwa sababu watu waliokulia ndani ya chama hicho ndiyo wamekuwa wakijenga makundi makubwa, kujuana, kupendeleana na kufumbiana macho, ukiniuliza nitasema CCM ya sasa inahitaji mtu “atakayekuwa anamuua nyani kwa kumfumbia macho”.

Yaani CCM inahitaji mtu asiyekulia ndani ya chama hicho na asiyejua ‘uhafidhina’, ‘uswahili’ wa wanaojiita “wenye chama”. Kwa lugha ya mtaani, chama hicho kinahitaji ‘mgombea kauzu’ na anayeweza kusimamia mambo ya nchi kwa matakwa ya raia bila kuyumbishwa na matakwa ya chama hicho, kama hayana tija. Mtu wa namna hii hawezi kuwa aliyekulia ndani ya CCM.

4. Mzoefu wa kufanya kazi nchini

Naiona sifa hii kama muhimu kwa CCM na isiyo na hatari kubwa. Kwamba inaweza kumteua mgombea mwenye uzoefu mkubwa katika kufanya kazi serikalini lakini awe anakijua chama hicho vizuri. Mtu wa namna hii anaweza kuwa na tija kwa chama hicho hasa ikiwa rekodi zake za utumishi ni nzuri na zenye tija.

5. Asiye na makundi na anayejua mahitaji ya makundi yanayosigana

Natambua kuwa tunakubaliana CCM iko kwenye mpasuko unaotokana na makundi na chama hicho hakina namna ya kufanya zaidi ya kuteua mgombea asiye na makundi na ambaye atakubaliwa na makundi mengine lakini ambaye ikiwa atachaguliwa, ataweza kuyalea makundi hayo kwa sababu anajua mahitaji yao na labda ataweza kutoa mahitaji ya makundi hayo ili kuyafanya yatulie na kutoisumbua Serikali na chama hicho.

Katika dhana hii ndipo wale wagombea ‘neutral’ huingia na kupata fursa ya kutuliza hali ya mambo.

Hatari ya sifa hii

Mgombea atakayeteuliwa kwa dhana ya kuwa ‘neutral’ anaweza kuwa hasimu mkubwa wa moja ya makundi yanayosigana na mapambano ya kutomuunga mkono yakaendelea. Au, mtu huyo atakayeteuliwa anaweza kuwa dhaifu kimtandao na kiuwezo kuliko yalivyo makundi yanayopambana. Kitakachojitokeza ni mpasuko mkubwa zaidi kuliko ambao ulikuwa unatatuliwa na huu wa pili unaweza kabisa kukosa mtu wa kuutatua. Kwa mtazamo wangu CCM, ilihitaji mgombea ambaye akiingia atasambaratisha makundi yote na labda kukiacha chama hicho ‘kipumue’.

6. Anayeweza kukemea rushwa huku

akiilinda CCM

Naweza kuthubutu kusema kuwa tangu alipoondoka Mwalimu Nyerere, CCM haijawahi kupata mgombea na hata kiongozi wa nchi aliyeonyesha nia ya dhati, moyo, malengo, kiu na uwazi katika mapambano dhidi ya rushwa. Moja ya mambo ambayo yanakiweka chama hicho kwenye hali mbaya kisiasa mwaka huu ni tuhuma kubwa za rushwa na ufisadi.

Hakika hapa ndipo CCM ilipo na mtihani mgumu zaidi, kwamba inaipasa kuteua mgombea msafi sana na asiye na madoa na ambaye anaichukia rushwa kuliko kifo na ameonyesha uwezo wa kupambana na rushwa katika rekodi zake, maneno yake na vitendo vyake.

Hatari ya sifa hii

CCM inapaswa kuita ‘nyeusi kama nyeusi na nyeupe vivyo hivyo’ kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Huu ni uchaguzi wa uamuzi pia na wa kuleta mapinduzi makubwa katika nchi na ushindani mkubwa kupita wakati wowote ule. Huu si mwaka wa kutaka mgombea mwadilifu na mpambanaji wa rushwa na wakati huohuo kutaka akilinde chama chake. CCM inahitaji mgombea ambaye atakuwa tayari hata kurudisha kadi ya CCM ikiwa chama chake kitaonekana kinaendekeza mtindo wa kutaka kulindwa kwa watu wake na kwa chama katika tuhuma kubwa za ufisadi na rushwa. Kufanya kinyume na hapo kutaendeleza yaleyale yaliyowakatisha Watanzania tamaa kwa miongo kadhaa iliyopita na adhabu yake kwa mwaka huu inaweza kuwa kubwa.

7. Maarufu, anayekubalika na anayeweza kuwa mshindi

CCM itahitaji mgombea ambaye yeye mwenyewe pia ni mtaji tosha wa kupata kura. Mwaka 2005 wakati chama hicho kilikuwa taabani kisiasa, kilikuja kuamshwa na nguvu, umaarufu na kukubalika kwa Jakaya Kikwete, kikajiandaa na ushindi wa kimbunga pamoja na kwamba kilisaidiwa sana na mifumo ya dola. Mwaka huu pia nadhani CCM itahitaji mtu wa namna hiyo ‘kama yupo’ ili kukiokoa. Maana ukizunguka vijijini unaona wananchi walivyochoka na wanavyohitaji mabadiliko.

Hatari za sifa hii

Kuteua mgombea maarufu kuliko chama kuna faida tu wakati wa kupiga kura na kushinda. Mara nyingi hakuna faida wakati wa kutekeleza ajenda za chama na kuwaletea maendeleo wananchi.

Sote tunakubaliana kuwa miaka 10 ya Kikwete imekuwa ya suluba kubwa, kwa mara ya kwanza tumeshuhudia (hasa miaka yake mitano ya mwisho), nchi ikishindwa kutekeleza baadhi ya bajeti za wizara kwa asilimia 50, fedha za miradi ya maendeleo zikitolewa kwa asilimia hadi 30 au 40 huku asilimia 70 hadi 60 zikikosekana katika miradi mingi, kuporomoka kwa uchumi, kuporomoka kwa shilingi na mambo mengine.

Inawezekana kuwa miaka 10 iliyopita Watanzania walichagua mtu maarufu na anayekubalika lakini hawakuangalia ana uwezo kiasi gani kuondoa umaskini, kuleta maendeleo, kurudisha nidhamu na uwajibikaji serikalini na kulinda kazi za raia. Kwa hiyo, yanayotokea leo, huenda ni madhara ya kuchagua mtu maarufu bila kuangalia umaarufu ule una tija gani kwa maendeleo na mahitaji ya Taifa.

8. Mwenye umri wa kati, msomi, mtulivu/mpole na mwenye busara

Katika kuweka hali ya mambo sawa, huenda CCM ikateua mgombea kwa sababu ya sifa hizi. Mtu wa umri wa kati ili kuwavutia vijana, wanawake na wazee (makundi yote ya kijamii) na katika chaguzi nyingine zote za nyuma CCM ilipitisha wagombea wake wakiwa na umri wa kati (chini ya miaka 60) na kufanikiwa.

Lakini pia, CCM inaweza kupitisha mgombea msomi ili aendane na kasi ya utendaji ya mabadiliko ya dunia na kuweza kuanzisha uongozi wa kisasa. Mahitaji ya kiongozi mwenye busara yanatokana na sababu kuwa nchi hii ni kubwa (Tanzania inalingana na nchi zote za Ulaya Magharibi, zikiwekwa pamoja).

Hii ni nchi yenye changamoto nyingi na viashiria vya migogoro vinavyoshika kasi. Inahitaji mtu mwenye busara za kutosha kuweza kuipeleka mbele.

Hatari ya sifa hii

Pamoja na mahitaji ya kiongozi mtulivu na mwenye busara, kiongozi huyo anapaswa asiwe mpole hata kidogo. Taifa letu lilipofika linahitaji rais mwenye sifa zozote zile lakini lazima awe mkali kama pilipili pale watendaji wanapojaribu kupindisha mambo fulani.

Asiishie tu kuwa mkali, pia achukue hatua stahiki kila mambo yanapoborongwa. Watu wengi ambao tunaambiwa wana busara kila nikiwaangalia nawaona kama wapole. Inawezekana kabisa kuwa Watanzania wengi wanaona kama busara na upole ni vitu vinavyokwenda pamoja.

Watu wapole wana matatizo makubwa katika usimamizi na kwa hakika binadamu anapaswa awe mpole katika mazingira yanayohitaji upole lakini awe mkali katika mazingira yanayohitaji ukali wa kiwango hichohicho.

9. Anayeweza kuupigania Muungano wa Serikali mbili kwa dhati

Sifa hii nayo isidharauliwe. Kwamba CCM itaitegemea katika kumpata mgombea urais wake. Tukumbuke kuwa CCM haiwakubali na kuwaamini viongozi wanaotaka Muungano nje ya mfumo wa Serikali mbili. Ndiyo kusema kuwa CCM kwenye suala la Muungano haitaki mjadala na haitaki wananchi wajiamulie wanataka wa namna gani.

Nasisitiza kuwa CCM inamtaka mtu ambaye anataka Muungano wa serikali mbili uendelee na si kinyume na hapo. Hii ni sera ya CCM na inaamini kuwa lazima iendelee kutekelezwa na wananchi wote tena bila kujali kuwa nchi hii sasa ina vyama vingi.

Hatari ya Sifa hii

Kitakachojitokeza ni kuwa, wananchi wengi wanaotaka kuwe na mjadala wa kitaifa wa muundo wa muungano wataendelea kudhibitiwa na hata kuonekana kama maadui wa Taifa kwa jambo la kimtizamo tu.

Kama nchi itatumia nguvu nyingi, akili nyingi na kila rasilimali kupigania mfumo wa serikali mbili na kusahau kuwa mahitaji makubwa ya wananchi ni maendeleo, naona CCM itazidi kushuka thamani na kupoteza mwelekeo. Kwa maoni yangu, CCM ingesaidiwa zaidi na mgombea ambaye atakuja na mtazamo huru juu ya muungano, hasa yule ambaye atakuwa tayari kuanzisha mjadala wa kitaifa ili wananchi waamue wanataka muungano wa namna gani.

Lakini pia, kuwaacha wagombea ambao wana sifa kubwa kuongoza nchi eti kwa sababu tu hawaamini sana katika serikali mbili itakuwa ni makosa makubwa. Sababu hii inaweza kukifanya chama hicho kichague mgombea mbovu kwa sababu atalinda serikali mbili.

10. Mwenye uzoefu na masuala ya kimataifa

Kwamba kwa namna dunia ilivyokumbwa na migawanyiko, mitanzuko na hata mabadiliko makubwa ya kidiplomasia, huenda CCM ikahitaji mtu mwenye uzoefu mkubwa wa masuala ya kimataifa kwa ngazi na kiwango ambacho chama hicho kitaona inafaa. Lengo litakuwa ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kufanya vizuri, kuheshimika na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.

Hatari ya sifa hii

Watu wengi waliobobea katika masuala ya kimataifa na kidiplomasia huamini katika dhana ya kushughulika kimataifa, kusafiri sana, kusaka misaada na marafiki kimataifa n.k. Ndiyo maana serikali inayomaliza muda wake imetumia muda mkubwa kufanya masuala ya kimataifa lakini hadi naindikapo hali ya nchi kimaendelea, kiuchumi na kijamii ndiyo kwanza inazidi kuwa mbaya.

Nadhani Taifa la Tanzania ya sasa linahitaji mtu mweledi wa kiwango cha kutosha kuweza kuongoza nchi na ambaye atakuwa na uwezo mkubwa zaidi katika kutengeneza fursa pana za kiuchumi ndani ya nchi, ambaye ataweza kuhamasisha wafanyabiashara wa ndani ya nchi wawekeze katika viwanda vidogovidgo na Serikali iwasaidie kusimamia sehemu ya mitaji ya viwanda vikubwa. Taifa linahitaji mtu ambaye atatumia muda wake mwingi akiwa mikoani na ofisini akisimamia utekelezaji wa maendeleo ya nchi yeye mwenyewe kuliko kusafiri kila uchwao kwenda nje ya nchi.

Kwa mtizamo wangu, kubobea katika masuala ya kimataifa huku ukikosa weledi muhimu wa namna ya kupandisha uchumi wa Taifa na wananchi ukiwa hapahapa ndani – hakuna tija yoyote katika Taifa maskini kama Tanzania.

Hitimisho:

Huu ni mwaka wa kusuka au kunyoa kwa CCM, chama hicho kikongwe huenda kinakabiliwa na changamoto kubwa kuliko wakati wowote ule kihistoria. Nguvu ya vyama vya upinzani imekuwa kubwa na haina mfano. Makosa ya CCM katika uteuzi wake ni jambo muhimu kwa vyama vya upinzani na ni suala la kujutia kwa CCM.

Sifa za mgombea wa CCM zina maana kubwa kama karata ya kutafuta ushindi wa chama hicho, na naamini kuwa kwa mwaka huu, kama CCM itaondoka madarakani, basi sababu mojawapo inaweza kuwa aina ya mgombea iliyempitisha.

Hata hivyo, nawatakia wana CCM na Watanzania wote tafakuri nzito juu ya mteule wake ambaye lazima tuseme ukweli kuwa, ikiwa atashinda uchaguzi, ndiye atakuwa Rais wetu wa awamu ya tano.

Advertisement