Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi amefariki

Thursday October 15 2015

Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya

Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi 

By Mwananchi Digital

Na Sauli Giliard
Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD) Dk Emmanuel Makaidi amefariki leo katika hospitali ya Nyangao mkoani Lindi leo mchana, familia yake yathibitisha.

Akithibitisha taarifa hizo, mke wa marehemu, Modesta Makaidi amesema mwanasiasa huyo machachari amefariki dunia baada ya kupatwa na shinikizo la damu na amefia hospitali ya Nyangao alipopelekwa kupatiwa matibabu.

Akihojiwa na moja ya vituo vya redio jijini Dar es Salaam, afisa habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Ukawa, Tumaini Makene amethibitisha kutokea kwa msiba huo.

Mbali na kukiongoza chama chake hicho, Dk Makaidi alikuwa akigombea ubunge jimbo la Masasi kupitia NLD ambacho ni moja ya vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mwanasiasa huyo machachari ndiye aliyekuwa mwenyekiti mwenza wa Ukawa na alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioonyesha msimamo mkali katika Bunge la Katiba.
Dk Makaidi alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara na ameshawahi kufanya kazi serikalini kabla kujitosa katika siasa.

Advertisement