Ajali ya ndege yavuruga mpango wa ubalozi wa Ethiopia nchini

Raia 25 wa Ethiopia wakiwa chini ya ulinzi katika ofisi ya Uhamiaji mkoani Tanga, Februari 14, 2017 baada ya kukamatwa wakituhumiwa kuingia nchini kinyume cha sheria baada ya kukamat-wa katika eneo la Mombo wakitokea Rombo, Kilimanjaro. PIcha na Maktaba

Muktasari:

Mipango iliyovurugika ya ubalozi huo kutokana na ajali ya ndege iliyoua watu 157, ni ile ya kuwasafirisha wahamiaji haramu 285 kutoka nchi hiyo ambao wamemaliza vifungo vyao katika gereza la Maweni mkoani Tanga, Tanzania.

Tanga. Ajali ya ndege aina ya Boeing 737 Max 8 iliyotokea nchini Ethiopia wiki hii, imevuruga mipango iliyokuwa imewekwa na Ubalozi wa nchi hiyo ya kuwasafirisha wahamiaji haramu 285 kutoka nchi hiyo waliomaliza vifungo vyao katika Gereza la Maweni, Tanga.

Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Nairobi, Kenya, ilianguka muda mfupi baada ya kuruka na kuua abiria na wafanyakazi wa ndege hiyo jumla yao ikiwa ni 157.

Imeelezwa kuwa awali, ilipangwa wahamiaji hao waanze kusafirishwa jana kwa mafungu ya watu 50 hadi watakapomalizika badala yake, safari yao itaanza leo na watalazimika kusafirishwa 30 kutokana na ndege waliyokuwa wamepangiwa awali kubadilishwa.

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Dady Ally aliliambia Mwananchi jana kuwa wahamiaji hao watasafirishwa kwa mabasi hadi Dar es Salaam na watapanda ndege kupelekwa Addis Ababa.

Ally alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa Balozi wa Ethiopia hapa nchini, Yonas Yosef Saube alipohudhuria maziko ya Wahabeshi wanane waliozikwa katika makaburi ya Neema jijini Tanga, Februari 13.

Maiti za Wahabeshi hao zilikaa chumba cha kuhifadhia maiti chaHospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo kwa siku 128.

“Maofisa kutoka ubalozi wa Ethiopia wapo jijini hapawakishirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mwisho za kuwasafirisha wahabeshi hao,” alisema Ally.