Aliyeibua hoja ya taulo za kike, ageukia nguo za ndani

Upendo Peneza, Mbunge wa viti maalum (Chadema)

Muktasari:

  • Baada ya kulalamikia bei ya taulo za kike (pedi) na kutaka Serikali ichukue hatua ili bei ipungue na kuwa msaada kwa watoto wa kike, mbunge Upendo Peneza sasa amegeukia nguo za ndani akitaka nazo zipunguzwe bei ili mabinti hasa wa vijijini waweze kuzinunua na kuzitumia kujistiri.

Dar es Salaam. Baada ya kupiga kelele kwa muda mrefu kuhusu gharama za taulo za kike hadi Serikali kufikia hatua ya kuziondolea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Upendo Peneza amegeukia suala la nguo za ndani.

Mbunge huyo wa viti maalum (Chadema), amesema gharama za nguo hizo, hasa maeneo ya vijijini, huwafanya mabinti kushindwa kununua na matokeo yake kuchangia hata taulo za kike zisitumike kwa usahihi.

Hali hiyo inamfanya mtoto wa kike ashindwe kujistiri vizuri wakati wa siku zake za hedhi.

Kufuatia hali hiyo Peneza alisema ipo haja kwa wizara ya fedha na mipango kuwa na dawati maalum la kijinsia litakalofanya kazi ya kuangalia masuala ya kijinsia na mwingiliano wake katika bajeti.

Kwa mujibu wa mbunge huyo uwepo wa dawati hilo utasaidia kuiwezesha Serikali kujua namna gani ya kusaidia upatikanaji wa bidhaa ambazo zinatumiwa na wanawake katika maisha yao ya kila siku.

“Serikali ifanye utafiti kuangalia bidhaa muhimu kwa wanawake mfano nguo za ndani zinaweza kuingizwa kwa gharama gani hadi kumfikia mhusika wa kawaida na ikiwezekana kuwa na bei elekezi ya kawaida kabisa ambayo watu wa hali zote wanaweza kumudu,” alisema.

Pia alitoa wito kwa wazazi kuhamasika kujua mahitaji ya mtoto wa kike na kumtengea fungu lake kwa ajili ya kupata mahitaji hayo.

Kuhusu taulo za kike alisema pamoja na kuondolewa kwa VAT bado taulo hizo zinauzwa kwa gharama ya juu kutokana kuwepo kwa kodi nyingine.

“Nilishaongea na kamishna wa (Mamlaka ya Mapato Tanzania) TRA kuhusu taulo hizi kuendelea kuwa bei juu akaniambia atafanyia kazi.”

“Ningeshauri Serikali iondoe kodi zote zinazohusika na uzalishaji na uingizaji wa taulo hizi ili ziuzwe kwa gharama nafuu na upatikanaji wake uwe wa uhakika hasa mashuleni,” aliongeza.

Juzi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alieleza kuwa ameanza kuchukua hatua kwa kumuandikia barua waziri wa fedha na waziri wa viwanda kuhusu taulo hizo kuendelea kuuzwa kwa gharama kubwa.

“Nimewaandikia waziri wa fedha na viwanda na biashara kuwataka waingizaji wa taulo za kike kupunguza bei ili kuhakikisha lengo la Serikali kuhakikisha wanawake wengi hasa wasichana walioko shuleni wanapata vifaa vya kujistiri kwa gharama nafuu, Sh2000 bado ni kubwa,”

Waziri huyo pia aligusia suala la ufungashaji wa taulo hizo kwa kile alichodai kuwepo na wafanyabiashara ambao wanazifunga kwa idadi ndogo ambayo haiwezi kukidhi mahitaji ya binti wakati wa hedhi.