Aliyetajwa na waziri Lukuvi kukwepa kodi ya ardhi afunguka

Mkurugenzi mtendaji na mmiliki wa Mbeya Hoteli ya jijini Mbeya, Shamash Walji

Mbeya. Mkurugenzi mtendaji na mmiliki wa Mbeya Hoteli ya jijini Mbeya, Shamash Walji amejitokeza na kuweka msimamo wake juu ya ulipaji wa deni la kodi ya ardhi analodaiwa baada ya Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kudai kuwa kiasi anacholipa hakiendani na ukubwa na eneo analomiliki na kulitumia.

Ijumaa Agosti 9, akiwa ofisini kwake jijini Dodoma, Waziri Lukuvi alimtaja Walji anayemiliki hoteli hiyo iliyopo katikati ya jiji la Mbeya kwamba ni miongoni mwa watu waliobainika kukwepa kodi ya ardhi.

Waziri huyo alisema hati ya umiliki wa eneo hilo ambalo ni kiwanja namba moja na mbili, kodi aliyoilipa tangu mwaka 2002 hadi sasa, hailingani na ukubwa wa eneo analomiliki.

Akizungumza na Mwananchi jana ofisini kwake jijini Mbeya, Walji alisema tangu walipomilikishwa hoteli hiyo miaka ya 2002, alikuwa akilipa kodi kama kawaida, lakini walikuwa wanalipa kwa ukubwa wa mita za mraba 506 badala ya 20,242.91.

Alisema hata yeye aligundua hilo baada ya taasisi mbalimbali za Serikali kuanza kumfuatilia, ndipo alipobaini kiasi cha kodi anacholipa ni kidogo ikilinganishwa na eneo analotumia na alipojiridhisha kwamba anaipunja Serikali, alikubali kulipa tofauti iliyopo na kuahidi kwamba yupo tayari kulipa deni lote kwa sababu hiyo ni kodi halali ya Serikali.

Aliishukuru Serikali kuibua suala hilo akisema, “sisi tulipogundua kuna kitu kama hicho, tulienda kwa mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kumwambia hatupo tayari kulumbana na Serikali, tupo tayari kulipa deni,” alidai Walji.

Alisema baada ya kufuatilia ilibainika pande zote mbili zilikubaliana kwamba kuna kosa lilifanyika huko nyuma.

“Nimeshangaa sana kutajwa kwamba nimekwepa kodi ya Serikali, mimi nimezaliwa Rungwe. Na sisi tuna viwanja zaidi ya 10 Rungwe na Mbeya na vyote tunalipia kodi bila usumbufu wowote, sasa iweje tukwepe kodi kwenye hili?

“Tupo tayari kulipa kodi hiyo kwa sababu ni kodi ya Serikali. Tunachoomba tu wenzetu Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, wafanye marekebisho ya makosa ambayo yalifanyika huko nyuma ambayo yanaweza kuwa ni ya kibidamu na watuletee mchanganuo mzima tangu tulipoanza kumiliki lile eneo, ili tujue tumelipa kiasi gani na tunadaiwa kiasi gani… tutalipa tu,” alisema mmiliki huyo. Alisema baada ya kuibuka kwa mkanganyiko wa kiwanja cha Mbeya Hoteli, alisema ataiomba Serikali kupitia wizara hiyo kuhakiki upya viwanja vyote anavyomiliki kuanzia ukubwa na matumizi yake ili aendelee kulipa kodi stahiki.

Kamishna wa ardhi msaidizi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Thadei Kabonge alisema ni jambo la busara kwa Walji kutambua kwamba eneo alililokuwa analipia kodi ni dogo ikilinganishwa na eneo analomiliki, hivyo kama alivyoomba kupelekewa hati ya madai yenye mchanganuo mzima tangu walipochukua eneo hilo, ofisi yake itafanya hivyo kesho kwa kumpelekea hati ya madai ya siku 14 na ndani ya muda huo atapaswa awe amelipa na si vinginevyo.

Alisema, “watapelekewa hati ya madai. Hii hati ya madai itaelezea kabisa tofauti kwa kila mwaka na atapewa siku 14 za kufanya malipo na baada ya hapo kama atakuwa hajalipa, hatua nyingine za sheria zitachukuliwa dhidi yake.”

Aliwataka wananchi ambao wanahisi kodi za ardhi wanazolipa haziendani na maeneo wanayotumia ni vyema wakafika kwenye ofisi za ardhi ili kufanya marekebisho stahiki na kuanza kulipa kodi inayopaswa.Katika mkutano wake na wanahabari, Waziri Lukuvi alisema mfanyabiashara Walji, “anamiliki ardhi hii tangu mwaka 2002, ardhi yake ina mita za mraba 20,234. Hii ilikuwa ni Mbeya Hoteli ameuziwa na Serikali na alipewa hati ya viwanja viwili vyenye ukubwa huo.”

Hata hivyo, Lukuvi alisema kwenye mfumo anaonekana analipia hati yenye mita za mraba 502 tangu mwaka 2002 alivyomilikishwa viwanja hivyo.

“Lakini amepatana na huyu kijana (mtumishi wa ardhi) amemuingizia kwenye mfumo wa kodi kiwanja chake kina mita za mraba 502… kwa kiwanja hiki alikuwa anatakiwa kulipa Sh6.3 milioni kila mwaka,” alisema.Alisema hadi Ijumaa alikuwa anapaswa kulipa Sh68.4 milioni kwa kipindi hicho.

Alisema kiwanja hicho kilichoko Mbeya Uzunguni katika mfumo wa wizara yake, kinaonyesha kinamilikiwa na Ramzan Warij.

“Huyu kijana aliyehusika na jambo hili kama yupo ndani ya Serikali, katibu mkuu atashughulika naye nimeshampatia jina. Huyu kijana yupo katika Serikali hadi leo amempunguzia ukubwa wa eneo kwa hiyo ameipotezea serikali zaidi ya Sh 60 milioni,” alisema.