Askari JWTZ wapaa na Dreamliner kulinda amani Sudan

Askari wa JWTZ wakipanda Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Airwing Dar es Salaa kuelekea  Darfur kwa ajili ya ulinzi wa amani, Jumla ya askari 217 wameondoka leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Askari 217 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  wameondoka leo Alhamisi Mei 16  kuelekea Sudan kwa ajili ya kulinda amani huku wakitumia ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)

Dar es Salaam. Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Alfred Kapinga amesema kitendo cha askari wa jeshi hilo kusafiri na ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwenda kulinda amani Sudan kinaonyesha namna ambavyo wanathaminiwa na Serikali.

Kapinga amesema hayo leo Alhamisi Mei 16 katika hafla fupi ya kuaga kundi la kwanza la  askari 217 wanaoelekea  Sudan, huku akisema miaka iliyopita askari hao walikuwa wakisafirishwa kwa ndege za kukodi.

Katika shughuli hiyo iliyofanyika katika uwanja wa ndege wa jeshi, Kapinga amesema hatua hiyo itawapa morali askari hao katika utekelezaji wa majukumu yao kwa sababu ni mara ya kwanza.

"Tumefarijika sana kutumia ndege ya ATCL kusafirisha askari wetu, kwanza katika kipindi cha miaka 12 tangu tuanze operesheni hizi za kulinda amani. Jambo hili litawaongezea morali askari kwa sababu wamepelekwa na chombo cha taifa," amesema Kapinga.

Mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema askari hao wameondoka na ndege aina ya Dreamliner ya shirika hilo itakayotumia saa 3 hadi kufika Sudan.

Mkuu wa kikosi hicho kinachokwenda Sudan, Luteni Kanali Khalfan Kayage ameishukuru Serikali na jeshi kwa kuwasafirisha kwa kutumia ATCL.