Auawa, atupwa kichakani

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole

Muktasari:

  • Hili ni tukio la pili ndani ya kipindi cha miezi miwili mwili wa mtu aliyekufa katika mazingira ya kutatanisha kupatikana wilayani Sengerema. Mei 25, 2019 mwili wa Tumaini Faustine (35), mkazi wa kijiji cha Nyakahako wilayani humo ulikutwa ukiwa umening’inia juu ya mti huku uchunguzi wa awali ukibaini alinyongwa kabla ya kutundikwa mtini

Buchosa. Debora Benado (37), mkazi wa kijiji cha Iligamba wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza aliyepotea siku nne zilizopita amekutwa akiwa amekufa na mwili wake kutupwa kichakani.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole ameiambia Mwananchi leo Jumanne Juni 18, 2019 kuwa tayari vyombo vya ulinzi na usalama vimeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na aliyekuwa mume wa marehemu, Nzito Lukansola anashikiliwa kwa mahojiano.

Akielezea tukio hilo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Chang’ombe, Petro Chimini amesema mwili wa marehemu uligundulika usiku wa kuamkia leo Jumanne baada ya wapita njia kugundua harufu kali kutoka kichakani na kutoa taarifa kwa uongozi.

“Mwili huo uliokuwa umeharibika umekutwa umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwa marehemu,” amesema Chimini

Amesema kutokana na mwili huo kuharibika ndugu wameruhusiwa kuendelea na taratibu za mazishi baada ya uchunguzi wa awali wa vyombo vya dola.

Akizungumzia mahusiano ya ndoa kabla ya kifo, Baba mdogo wa marehemu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Masinde amesema alikuwa ametengana na mumewe miaka miwili iliyopita na kifo chake kumeiachia familia majonzi na mzigo wa kuwalea na kuwatunza watoto wake saba aliowaacha.