Azaki 154 zapatiwa Sh11.7bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo

Muktasari:

  • Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara afungua milango kwa Azaki 154 zinazotakiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwaripoti watendaji na viongozi watakaokuwa na nia ya kuwakwamisha.

Dodoma. Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amezitaka Azaki za kiraia 154 zilizopata ruzuku kwa mwaka 2019, kuwaripoti watendaji na viongozi mbalimbali ambao watakuwa kikwazo kwao katika utekelezaji wa miradi  ya maendeleo.

Azaki za Kiraia 154 kutoka Tanzania Bara na Visiwani, zimepatiwa Sh11.7bilioni zikiwa ni ruzuku za miradi watakayotekeleza ili wanufaika wafikiwe na kufaidika nayo.

Waitara alitoa agizo hilo jijini hapa jana Jumamosi Juni 8,2019 alipokuwa akifungua mkutano wa wakurugenzi wa Azaki na kuzindua kazi ya kusaini mikataba ya ruzuku kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Tanzania Bara na Visiwani.

“Nimeelezwa kuwa kwa mwaka huu, Foundation for Civil Society itatoa ruzuku ya takribani Sh11.7 bilioni kwa Azaki 154 Tanzania Bara na Visiwani ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yenu, sasa kwenye utekelezaji wa miradi hiyo, waripoti kwangu wale ambao watakuwa na lengo la kuwakwamisha, lakini na nyiye mnatakiwa kufuata taratibu zote  za kisheria,” alisema  Waitara.

Majukumu yatakayotekelezwa na fedha hizo ni kuwezesha wananchi kufahamu mfumo mzima wa bajeti ya Serikali na hivyo kufuatilia mapato na matumizi pamoja na miradi mingine katika sekta ya elimu, maji, afya na kilimo.

Alisema kupambana na ukatili wa kijinsia na watoto, kutetea haki za watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kunufaika na mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na halmashauri nchini.

 

Waitara alisema ipo miradi ya kuwezesha elimu ya ujasiriamali kwa vijana na kuwezesha kunufaika na mikopo ya asilimia nne inayotolewa na halmashauri, kuwezesha elimu ya haki ya ardhi kwa wanawake na miradi inayochangia utengemano na Amani katika jamii kama utatuzi wa migogoro.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Francis Kiwanga alisema shirika hilo limetoa orodha ya asasi za kiraia 154 zilizofuzu kupokea ruzuku ili kutekeleza miradi mbalimbali kuanzia mwaka huu.

Alisema orodha hiyo inatokana na mchakato wa upitiaji miradi 1,000 iliyopokelewa mwaka jana, huku akitaja miradi  itakayopewa ruzuku inagusa maeneo ya utawala bora, ujenzi wa amani na utatuzi wa migogoro, uboreshaji maisha na kukuza uchumi.

Hata hivyo, amezitaka Azaki kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na thamani ya fedha.

Mkurugenzi wa taasisi ya Tusonge, Aginata Rutaza ameiomba Wizara ya Tamisemi kuweka utaratibu wa kuomba kibali cha kutekeleza miradi kupitia mtandaoni badala ya kufika ofisini moja kwa moja.