Azunguka kuuza ice cream na mwanaye baada ya mke kumkimbia

Muktasari:

  • Baada ya kukimbiwa na mke, Ayub Ramadhan hakuwa tayari kumpeleka mtoto wake wa miaka mitatu kwenda kulelewa na bibi na babu, badala yake ameamua kuzunguka naye mitaani akitafuta wateja wa kununua ice cream, biashara inayomuingizia kipato cha kuendesha maisha.

Moshi. Mara nyingi mwanamume anapoachiwa mtoto na mzazi mwenzake, humpeleka kwa mama yake mzazi kumsaidia kumlea, lakini si kwa Ayubu Ramadhan.

Muuza ice cream huyo, anayelazimika kuzurura mitaa kadhaa kutafuta wateja, ameamua kumlea mwenyewe, bila ya msaidizi wa kazi wa ndani.

Na kutokana na kuzura mitaani na mtoto wake wa kiume wa miaka mitatu na miezi sita wakati akisaka wateja, Ayubu amekuwa maarufu mjini Moshi.

Kuna wakati inamlazimu kumtandikia mtoto huyo kivulini pembezoni mwa barabara ili alale, wakati akiendelea kuuza ice cream, huku wanafunzi wa shule za msingi wakimsaidia chakula cha mtoto.

“Kutokana na kukosa mtu atakayenisaidia kumlea inanilazimu kwenda naye kwenye kibarua changu hicho ambacho ndicho kinanipa maisha,” alisema Ayubu.

Alisema ameshazoea maisha hayo kwa sasa.

“Natoka asubuhi saa 1:00 asubuhi kufuata mzigo na ni lazima nitoke na mwanangu kutokana na kukosa mtu wa kunisaidia kukaa naye, nazunguka naye barabarani muda wote na ikifika 12 jioni tunarudi nyumbani,” alisema alipozungumza na Mwananchi.

Ayubu alifunga ndoa Desemba 12, 2013 na mkewe alikuwa akiishi wilayani Kondoa, Dodoma hadi Mei 2017 walipotengana.

Anasema akiwa na mzazi mwenzie, alikuwa akifanya kazi kwenye mashine ya kusaga nafaka mjini Moshi na alikuwa akituma fedha za matumizi Kondoa.

Fedha za mtoto zageuka nauli

Ayubu anasema aliamua kutembelea familia yake Kondoa Mei 2017 na wakati anaondoka alimuachia mkewe fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya familia na yale ambayo ni maalumu kwa mtoto.

Hata hivyo, alidai mzazi mwenzake hakutumia fedha hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa, badala yake aliigeuza kuwa nauli ya kurudi kwa wazazi wake na kumtelekezea mtoto huyo aitwaye Ramadhani.

“Nakumbuka kipindi hicho nilienda kuitembelea familia yangu. Mke wangu akaniambia chukua mzigo wako (mtoto). Akaondoka na kuniachia mtoto akiwa na mwaka mmoja na miezi mitano,” alisema.

“Baada ya kuondoka wazazi na ndugu wa karibu walijitahidi kumuomba arudi kumlea mtoto, lakini alikataa. Sikuwa na njia nyingine nikaamua kubeba jukumu la kuwa baba na hapo hapo mama.

“Niliamua kurudi Moshi na mtoto wangu na kutafuta kibarua kingine ndipo nikapata kazi hii ya kuuza ice cream mwezi huohuo watano.”

Anasema kwa siku anaweza kuingiza Sh5,000 hadi Sh6,000 ila msimu wa baridi huambulia Sh2,000 na wakati mwingine anaweza kutopata kitu.

“Pesa hii ndiyo naitumia kuishi mimi na mtoto wangu,” anasema.

Changamoto inayomkabili

Ayubu anasema mtoto wake anakabiliwa na changamoto kama kutopata chakula cha uhakika wakati wanapokuwa katika biashara kwa vile baadhi ya maeneo hayana sehemu zinazouza chakula.

Lakini anasema vijana walinzi wanaopika eneo la jirani na shule ya msingi Kibo anakouzia ice cream, mara nyingi huwasaidia chakula kwa kuchangia fedha kidogo.

“Pamoja na kukosa chakula cha uhakika lakini wakati mwingine damu humtoka puani wakati wa jua kali kwa kuwa hushinda juani muda mrefu,” alisema Ayubu.

Lakini Ayubu hafurahii hali hiyo ya kushinda na mtoto mchana kutwa. Anatafakari uwezekano wa kupata shule ya awali.

“Ninaona akipata shule ya awali itanisaidia kutafuta kipato kwa uhuru zaidi na pia itamsaidia mtoto asizidi kuathirika na mazingira tunayopitia, hasa haya ya kukosa chakula mchana,” alisema.

Ayubu ameomba wasamaria wema wanaoweza kumsaidia, wafanye hivyo kupitia namba za mwakilishi wa kampuni ya Mwananchi mkoa wa Kilimanjaro.

Mwajiri azungumza

Hatibu Ramadhani, mwajiri wa Kijana huyo, alisema baada ya Ayub kumueleza matatizo aliyopata, ilimuumiza sana na akaamua kumsaidia.

“Jambo pekee nililoweza kumsaidia ni kumpatia kazi ambayo ndiyo inayomsaidia yeye na mtoto wake kujikimu kimaisha kwa sasa. Ninatamani na Watanzania wengine waguswe na hili,” alisema.

Mkazi wa Njoro, Josephine Mushi, anasema alikuwa akijiuliza maswali mengi kila anapomuona kijana huyo na mtoto.

“Siku moja nilijawa na ujasiri nikamuuliza ndio akanipa hiyo hadithi yake. Kwa kweli niliumia sana. Hapa ndipo nilipojua wanawake tunatofautiana. Binafsi singeweza kufanya kitendo hiki,” alisema.

Mwanamke huyo anasema kwa jinsi uchungu wa kumzaa mtoto ulivyo, hatamani kumuacha mtoto wake kwa mtu hata kama ana umri wa miaka zaidi ya saba.