Bei ya petroli, dizeli yapaa tena nchini

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei mpya za mafuta mwezi Desemba inasema bei elekezi kwa mwezi huu inaonyesha petroli imepanda kwa asilimia 1.66, dizeli (2.11) na mafuta ya taa asilimia 3.85.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei mpya za mafuta mwezi Desemba ambazo zimeendelea kupanda tena.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa inasema bei elekezi kwa mwezi huu inaonyesha petroli imepanda kwa asilimia 1.66, dizeli (2.11) na mafuta ya taa asilimia 3.85.

Taarifa hiyo imesema pia lita moja ya petroli imeongezeka kwa Sh40, dizeli Sh50 na mafuta ya taa Sh88. Bei hizo zilianza kutumika rasmi jana.

Kwa bei hizo mpya wanunuzi wa Dar es Salaam sasa watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,436, dizeli Sh2,436 na mafuta ya taa Sh2,368.

Kwa upande wa Arusha lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh2,492, dizeli Sh2,437 na mafuta ya taa Sh2,282.

Kigoma watanunua petroli kwa Sh2,668, dizeli Sh2,667 na mafuta ya taa Sh2,600, wakati mkoani Mbeya petroli sasa inauzwa kwa Sh2,543, dizeli Sh2543 na mafuta ya taa yanauzwa Sh2,475.

Mkoani Ruvuma petroli inauzwa kwa Sh2,560, dizeli Sh2,429 na mafuta ya taa Sh2492 wakati kwa Mkoa wa Mwanza petroli inauzwa kwa Sh2,586, dizeli Sh2586 na mafuta ya taa kwa Sh2,518.

Hata hivyo, Ewura imesema kupanda kwa bei ya bidhaa hizo kunatokana na kupanda kwa mafuta katika soko la dunia.

Katika bei elekezi iliyotangazwa na Ewura mwezi Novemba lita moja ya petroli ilikuwa ikiuzwa Sh2,396, dizeli Sh2,385 na mafuta ya taa Sh2,280.

Taarifa ya ufafanuzi wa bei iliyotolewa na mamlaka hiyo jana jioni ilisema bei za mafuta ghafi katika soko la dunia zimekuwa zikiongezeka mwezi hadi mwezi kutoka Dola 75 za Marekani kwa pipa hadi Dola 81 mwezi Oktoba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwenendo wa bei za mafuta safi nao umekuwa ukilingana na ule wa mafuta ghafi, ingawa kwa viwango vya mabadiliko hutofautiana kutokana na gharama za kusafisha mafuta ghafi pamoja na tofauti ya mahitaji ya mafuta husika ya petroli, dizeli au ya taa.